KUENDANA NA KASI YA MABADILIKO : MADEREVA WA SERIKALI KUHAMASISHWA KUPITIA MAFUNZO YA TEKNOLOJIA YA KISASA

News Image

Posted On: September 02, 2025

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, amewataka madereva wa Serikali kupatiwa mafunzo ya teknolojia ya kisasa ya magari inayoendana na kasi ya mabadiliko ili kuongeza ufanisi wa kazi zao na kulinda rasilimali za umma.

Akizungumza leo tarehe 02 Septemba wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Nne la Chama cha Madereva wa Serikali (CMST) lililofanyika jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa madereva kupewa mafunzo ya mara kwa mara, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.

Mheshimiwa Majaliwa amesema ni muhimu madereva wa Serikali kupatiwa elimu inayoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya kisasa yakizingatia matumizi ya mitambo, vifaa vinavyosaidia kufanya kazi na mabadiliko ya mashine ambapo TEMESA imepatiwa jukumu hilo la kutoa mafunzo hayo kwa madereva.

“Madereva wetu wapate mafunzo ya kitaalamu hasa ya mabadiliko haya ya kisayansi na kidigitali, mafunzo haya yafundishe sheria, namna ya utunzaji wa afya zao pamoja na muonekano wao”alisistiza waziri mkuu.

Aidha ameipongeza wadau mbalimbali kwa kuendelea kuwashika mkono madereva katika kongamano hilo ambapo TEMESA ikiwa ni mmoja wa wadhamini wa kongamano hilo.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, amesema madereva wa Serikali ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za utumishi wa umma, akisisitiza kuwa nidhamu na uadilifu ndiyo msingi wa heshima na mafanikio ya kada hiyo.

Waziri Ulega alibainisha kuwa Serikali inaweka ustawi wa madereva kuwa moja ya vipaumbele vyake muhimu.

“Sisi kama Serikali tutahakikisha madereva wanafanya kazi katika mazingira bora. Wakihudumiwa vizuri, watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kwa moyo wa kujituma,”

alisisitiza Waziri Ulega.

Aidha, alisema kuwa mkutano huo una lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili madereva, kubadilishana uzoefu wa kazi, pamoja na kuimarisha mshikamano na weledi katika utendaji wao wa kila siku.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST), Bw. Castro Nyabange, amepongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa katika kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, wakiwemo madereva.