SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA KARAKANA ZA TEMESA
Posted On: June 22, 2023
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imeendelea kufanya maboresho kwenye karakana zake kwa lengo la kuongeza tija na ubora wa huduma kwa Taasisi za Umma na binafsi zinazohudumiwa na karakana hizo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Hassan Karonda wakati akizungumza kwenye kipindi cha Ijue TEMESA kinachoandaliwa na Kitengo cha Masoko na Uhusiano cha Wakala huo.
Mhandisi Karonda amesema, maboresho hayo yanajumuisha ukarabati wa karakana za zamani ambazo zimeanza kuchoka, ununuzi wa vitendea kazi vipya vya karakana, mafunzo kwa mafundi wa karakana ili kuweza kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea kukua siku hadi siku pamoja na ujenzi wa karakana mpya za Mikoa na Wilaya.
‘’Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/2023, TEMESA inaendelea kufanya ukarabati katika karakana za Mikoa mitano ukiwemo Mkoa wa Arusha, Mara, Tabora, kigoma na Mkoa wa Mtwara, huku Karakana za Mikoa ya Dodoma na Pwani zikitarajiwa kuanza kufanyiwa ukarabati mkubwa awamu ya pili ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni, Serikali pia imetenga fedha kwenye bajeti yake kwa mwaka ujao wa fedha wa 2023/2024 kwa ajili ya kukarabati karakana za Mikoa ya Kagera, Morogoro na Mkoa wa Tanga.’’ Amesema Mhandisi Karonda na kuongeza kuwa pamoja na ukarabati wa karakana unaoendelea kufanyika, Serikali pia imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa karakana mpya ambapo amezitaja karakana hizo kuwa ni Karakana ya Mkoa wa Simiyu ambayo ujenzi wake utaanza kwa awamu ya pili baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza, karakana ya Mkoa Geita ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua ya (design) kubuniwa huku mkandarasi akiwa amekwishapatikana pamoja na karakana za Mikoa ya Njombe, Songwe na Katavi.
Akizungumzia kuhusu mikataba ambayo Wakala huo umeanza kuingia na Washitiri wake kwa ajili ya kufanya matengenezo kinga ya magari, mitambo na vifaa mbalimbali vya umeme ikiwemo kangavuke, Mhandisi Karonda amesema kuwa Wakala umeingia mikataba ya namna hiyo kwa lengo la kurahisisha kazi baina ya Wakala na Taasisi husika kwani TEMESA kwa kufahamu mahitaji ya Taasisi husika ya matengenezo ya magari yake, inakuwa tayari imekwishajiandaa kwa vipuri vya kutosha vya magari husika, bei ya vipuri na hivyo kuokoa muda mwingi wa utendaji wa kazi.
‘’Kwenye hili zoezi la kuingia mikataba, tunakuwa na orodha kamili ya yale mahitaji, yani vifaa walivyokuwa navyo, mitambo, kangavuke na magari, kwahiyo inakuwa ni rahisi kwa sisi katika kuagiza vile vipuri mfano (fast moving items) vipuri vinavyotumika mara nyingi vya matengenezo kinga, tunakuwa navyo tayari, na hata vipuri vya matengenezo makubwa tunakuwa navyo kwasababu tunajuwa mahitaji yao, hii inarahisisha muda wa kuhudumia iyo gari kuliko yule anaekuja kwa kushtukiza’’. Amesema Mhandisi Karonda
Aidha Mhandisi Karonda amesema kuwa TEMESA ina mkakati wa kuongeza ujuzi kupitia watengenezaji wa magari kwa kuhakikisha wanashirikiana na TEMESA namna bora ya kutengeneza magari hayo kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa mafundi na wataalamu wa TEMESA ili magari hayo yaweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu na kuleta tija iliyokusudiwa na Serikali.
Mkurugenzi amesisitiza kuwa Serikali kila mwaka imekuwa ikitenga fedha katika bajeti zake kwa ajili ya Wakala huo kununua vitendea kazi vya karakana ambapo vitendea kazi hivyo vimekuwa vikiurahisishia Wakala majukumu yake ya kila siku kwa kuufanya ufanye kazi kwa ubora na ufanisi mkubwa, Mhandisi Karonda ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za TEMESA.