​SERIKALI YAKAMILISHA UJENZI WA VIVUKO VIPYA VIWILI

News Image

Posted On: September 22, 2025

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imekamilisha ujenzi wa vivuko vipya viwili kati ya sita vilivyokuwa vinajengwa katika yadi ya Songoro Marine iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza. Vivuko hivyo viwili ni MV. BUKONDO ambacho kinakwenda kutoa huduma kati ya Bwiro na Bukondo Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza na kivuko MV. UKEREWE ambacho kinakwenda kutoa huduma kati ya Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Nansio Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza.

Ujenzi wa vivuko hivyo ulianza mnamo Oktoba, 2022 na ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 ambapo Serikali iliahidi kujenga vivuko vipya sita ambavyo vitakwenda kutoa huduma ya usafiri wa vivuko katika maeneo ambayo yalikuwa na changamoto ya usafiri.

Akizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kushuhudia zoezi la kushusha kwenye maji kivuko MV. UKEREWE na kivuko MV. BUKONDO ambalo lilifanyika kwa ukamilifu mkubwa, Mhandisi Lukombe King'ombe, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko TEMESA alisema tayari vivuko hivyo viwili vinaelea kwenye maji ndani ya Ziwa Victoria vikisubiri kufanyiwa majaribio kabla ya kufanyiwa uchunguzi wa mwisho ili viende kutoa huduma katika maeneo vilivyopangiwa.

“Kivuko cha MV. UKEREWE kitakwenda kutoa huduma eneo la Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, wakati hiki cha MV. BUKONDO kitakwenda kutoa huduma kati ya Bwiro na Bukondo Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza.” Amesema Mhandisi King’ombe na kuongeza kuwa TEMESA kupitia Wizara ya Ujenzi inaishukuru Serikali kwa kuwezesha kukamilika kwa miradi hiyo mikubwa miwili.

“Tunayo furaha kusema kuwa miradi hii imekamilika na wananchi wa Bwiro na Bukondo na Kisorya Rugezi kaeni mkao wa kula vivuko vinakuja, tunaishukuru sana Serikali kwa kuiwezesha TEMESA kutekeleza miradi hii kwa ufanisi, vyombo vyote hivi viwili (MV. UKEREWE na MV. BUKONDO) vimefungwa vifaa vya kisasa ambavyo vinatumika kwenye vyombo vya majini, hatua tuliyofikia wataalamu watafanya kazi za mwisho ambazo ni kumalizia rangi, pamoja na kazi ndogo na baada ya hapo vivuko vitakwenda maeneo husika kutoa huduma." Amesema King'ombe.

Mhandisi King’ombe ameongeza kuwa Kivuko cha MV. BUKONDO kinao uwezo wa Tani 100, kinabeba abiria 200 na magari madogo 10 wakati kivuko cha MV. UKEREWE kinao uwezo wa Tani 170, kinabeba abiria 800 na magari 22.

Kivuko MV. BUKONDO kimeigharimu Serikali shilingi Bilioni 4.5 mpaka kukamilika kwake wakati kivuko MV. UKEREWE kimegharimu shilingi Bilioni 5.5.