SERIKALI YATOA TRILIONI 1.319 KUIMARISHA MIUNDOMBINU, ULEGA AELEZA MAFANIKIO SEKTA YA UJENZI
Posted On: March 24, 2026
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa Serikali imeendelea kupiga hatua katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo hadi kufikia Machi 2026, jumla ya shilingi trilioni 1.319 tayari zimetolewa kwa ajili ya miradi iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na makadirio ya mwaka 2026/2027 kwa fungu 98 la Wizara ya Ujenzi Machi 23, 2026 Mkoani Dodoma, Ulega alieleza fedha hizo ni sawa na asilimia 72.80 ya bajeti iliyoidhinishwa na kubainisha mafanikio yaliyopatikana hadi kufikia Machi, 2026.
Waziri Ulega akiizungumzia Sekta ya vivuko, ameeleza kuwa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umekamilisha maegesho ya kivuko ya Ijinga Kahangala, Bwiro Bukondo pamoja na Kisorya–Rugezi–Bukimwi, sambamba na kukamilisha ujenzi wa kivuko MV. UKEREWE kitakachotoa huduma kati ya Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, vile vile Serikali imekamilisha ujenzi wa kivuko MV. BUKONDO kitakachotoa huduma kati ya Bwiro na Bukondo Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza pamoja na kukamilisha ukarabati wa boti ya dharura ya MV. TANGAZO inayotoa huduma Mkoani Mtwara..
Ulega alisisitiza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Ujenzi itahakikisha inatekeleza kwa vitendo maono na dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu kupitia miundombinu bora, salama na yenye tija.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso, aliipongeza Wizara hiyo kwa juhudi zake katika kusimamia na kutekeleza miradi ya kimkakati, hususan ujenzi wa vivuko, barabara na madaraja unaorahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria nchini.