UKARABATI KIVUKO CHA MV. TANGA WAFIKIA HATUA NZURI
Posted On: August 29, 2022
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA inaendelea na utekelezaji wa miradi ya ukarabati wa vivuko nchini ambavyo muda wake wa kukarabatiwa umefika ili viendeelee kutoa huduma vikiwa katika hali ya usalama, katika muendelezo huo, kivuko cha MV TANGA kinachotoa huduma kati ya Pangani na Bweni Wilayani Pangani Mkoani Tanga ni miongoni mwa vivuko ambavyo vinaendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa
Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ukarabati wa kivuko hicho unaoendelea katika eneo la Pangani Mkoani Tanga, Meneja wa vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe amesema ukarabati huo unahusisha kuondoa mabati ambayo yamekwisha haribika sehemu za abiria na magari yanapopaki yakiingia ndani ya kivuko pamoja na chini ya kivuko, viti vya abiria, vifaa vya uokozi ikiwemo majaketi ya kujiokoa pamoja na maboya ya kujiokoa, kuondoa milango ya mbele na nyuma ya kivuko (ramps), kufunga viongoza kivuko vipya (navigation systems) pamoja na kupaka rangi kivuko hicho mara baada ya ukarabati wake.
Naye Mkuu wa Kivuko cha Pangani Mhandisi Abdulrahman Ameir akizungumza wakati wa ukaguzi huo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha huduma za vivuko nchini kwa kuendelea kuvifanyia ukarabati vivuko vyake kote nchini na kuahidi kusimamia kwa ukaribu kuhakikisha mkandarasi anamaliza kukarabati kivuko hicho kwa ufanisi na katika muda uliopangwa na kukirejesha kivuko hicho kutoa huduma haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa Mkandarasi anayefanya ukarabati huo, Dar es Salaam Merchant Group, kivuko cha MV.TANGA kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.