GERSON MSIGWA AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA VIVUKO VIPYA VINAVYOJENGWA NA SERIKALI MWANZA
Posted On: May 07, 2025
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa vivuko vipya vitano kati ya sita vinavyoendelea kujengwa na Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoani Mwanza. Vivuko hivyo vipya vitano vinajengwa na Mkandarasi Songoro Marine Boatyard katika yadi yake iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza.
Ziara hiyo ya kutembelea miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika Jiji la Mwanza, imefanyika Mei 2,2025 imeongozwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuwahabarisha wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Msigwa amesema miradi hiyo inalenga kuondoa changamoto za usafiri na usafirishaji, sambamba na kuchochea ukuzaji wa uchumi katika ukanda wa Ziwa Victoria na taifa kwa ujumla. Msigwa amesema dhamira ya Serikali ni kuwezesha wananchi wake kujiletea maendeleo kwa kuweka miundombinu ya kisasa inayochangia katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.
Msigwa ameongeza kuwa Rais Samia anaguswa sana na changamoto ya usafiri kwa wananchi wa maeneo yote ya maziwa ikiwemo Kanda ya Ziwa na kusema kuwa miradi kama hiyo inafanyika pia katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.
“Miradi hii ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika kuleta maendeleo ya kweli na ya haraka kwa wananchi,tunataka wananchi wote wajue kinachoendelea na wawe sehemu ya mafanikio haya,” amesema Msigwa.
Baadhi ya miradi mingine iliyotembelewa na Msemaji Mkuu ni pamoja na ujenzi wa daraja la Busisi, pamoja na meli ya MV Mwanza ambayo kwa sasa imekamilika kwa asilimia 98.