''VIVUKO VIPYA MWANZA KUKAMILIKA MWEZI SEPTEMBA, 2025,'' ULEGA

News Image

Posted On: June 09, 2025

Ujenzi wa vivuko vipya vitano vinavyoendelea kujengwa na mkandarasi Songoro Marine katika yadi ya Songoro iliyoko Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba mwaka huu wa 2025. Hayo yamebainishwa Tarehe Juni 8, 2025 na Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega Mkoani Mwanza wakati alipokuwa akielezea mafanikio katika Sekta ya Ujenzi kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia kwa waandishi wa habari ambapo amesema vivuko hivyo vipya vitano vinavyojengwa Mkoani Mwanza kati ya sita, vitakapokamilika vinatarajiwa kwenda kutoa huduma katika visiwa vilivyoko Mkoani Mwanza na maeneo ya Kanda ya Ziwa.

Waziri Ulega ameyataja maeneo vivuko hivyo vitakwenda kutoa huduma kuwa ni eneo la Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza ambapo kivuko kipya cha MV. UKEREWE kinatarajiwa kupelekwa kitakapokamilika, ametaja pia kivuko kipya cha MV. KOME III kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Nyakarilo na Kome Halmashauri ya Wilaya Buchosa, kivuko kingine kipya ni MV. BUKONDO kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Bwiro na Bukondo Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, amekitaja kivuko kipya kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Ijinga na Kahangala Wilayani Magu Mkoani Mwanza, Waziri Ulega amekitaja pia kivuko kipya kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Buyagu Wilayani Sengerema na Mbalika Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza pamoja na kivuko kingine kipya cha sita ambacho ni kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati Wilayani Kibiti Mkoani Pwani ambacho kitakwenda kusaidiana na kivuko MV. KILINDONI ambacho kinatoa huduma katika eneo hilo.

''Katika kipindi cha Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na kinara wetu jemedari Daktari Samia Suluhu Hassan, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imeiwezesha TEMESA kuanza ujenzi wa vivuko vipya vitano katika eneo hili la Ziwa Victoria peke yake na kimoja katika bahari ya Hindi kile cha kutoka Nyamisati kwenda Mafia, vivuko hivyo vinatarajiwa kukamilika Septemba, 2025.'' Alisema Waziri Ulega na kuongeza kuwa Wizara inashukuru kwa kupata maelekezo kutoka kwa Mhe. Rais ambaye anataka Serikali ambayo inashirikiana na Sekta binfasi katika utoaji wa huduma.

''Dkt. Samia Suluhu Hassan ni muumini sana wa Serikali inayoshirikiana na Sekta binafsi na ndiyo maana alitupa maelekezo kama Wizara si kwamba kila kivuko tufanye sisi wenyewe kama Serikali badala yake tuangalie uwezekano wa kushirikisha na Sekta binafsi na ndiyo maana pale Dar es Salaam tulimualika Azam Marine aje kushirikiana nasi akatuitika na tunayo furaha kubwa sana kwamba Azam Marine anasaidiana na Serikali kuvusha watu pale eneo la Magogoni Kigamboni kwa kitumia zile Sea Taxi na imeondosha sana msongamano,'' amesema Waziri Ulega na kuongeza kuwa Serikali na Watanzania wenyewe ni mahodari sana wa kutatua changamoto zinazowakabili