USIMIKAJI WA MIFUMO YA UMEME KATIKA JENGO LA WIZARA YA UJENZI MTUMBA UNAFUATA MIONGOZO YA KIMATAIFA
Posted On: August 29, 2024
Meneja wa TEMESA Kikosi cha Umeme, Mha.Pongeza Semakuwa amesema, mradi wa usimikaji wa mifumo ya umeme katika jengo la Wizara ya Ujenzi na Wizara Uchukuzi unaendelea vizuri na mafundi wamekuwa wakitimiza majukumu yao kwa kufuata miongozo ya kihandisi ya ndani ya Nchi na ya kimataifa.
Mhandisi Pongeza ameyasema hayo leo 29 Agosti, wakati alipotembelea mradi huo kukagua maendeleo ya usimikaji wa mifumo wa jengo la wizara ya ujenzi na wizara ya uchukuzi lililopo katika mji wa kiserikali Mtumba jijini Dodoma ambapo TEMESA imepewa jukumu la usimikaji wa mifumo ya umeme, TEHAMA,vizimia moto na viyoyozi.
Mhandisi Pongeza amesema kwa upande wa TEMESA, hadi kufikia sasa wamekwishaweka miundombinu ya awali kwa ajili ya kupitisha nyaya, viyoyozi na kufunga mabomba yatakayochukua nyaya kutoka kwenye seva na kusambaza kwenye vyumba vya matumizi.
“Sisi kama Wakala wa Ufundi na Umeme tumeshaanza kazi kwenye upande wa umeme, viyoyozi na upande wa TEHAMA ambapo kwa upande wa umeme tumeshaweka miundombinu ya awali kwa ajili ya kupitisha nyaya lakini pia kwa upande wa viyoyozi tumesimika miundombinu ya awali”.
Mhandisi pongeza amesema kazi hizo zitakamilika ndani ya mkataba na vifaa vyote vya mradi vinavyotegemewa kufanyia kazi awamu ya pili vimeshafikishwa eneo la kazi.
“Mpango wetu ni kuweza kukamilisha kazi hii ndani ya mkataba na kama mnavyojionea vifaa vyote vya mradi tumeshavifikisha site yaani kwa maana ya jenereta, transfoma na nyaya ambavyo kwa kiasi kikubwa tunavitegemea kufanyia kazi katika awamu ya pili”alisistiza Mhandisi.
Aidha, ameishukuru serikali ya awamu ya sita, vikosi vya ujenzi, TBA pamoja na Wizara ya Ujenzi, kwa kuiamini TEMESA na kuendelea kuipatia kazi na kuahidi kufanya kazi kwa mujibu wa miongozo na taratibu zilizopo.