DAC DODOMA AIPONGEZA TEMESA KWA HUDUMA YA UKAGUZI WA MAGARI WILAYANI DODOMA

News Image

Posted On: November 14, 2025

Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma Bi. Sakina Mbugi ameipongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa hatua ya kupeleka huduma ya ukaguzi wa magari moja kwa moja katika ofisi za Serikali za Serikali za wilaya ya Dodoma Pamoja na na ofisi za halmashauri ya jiji, hatua iliyolenga kuhakikisha magari yote yanayotumika na taasisi za umma yanakuwa salama na katika hali bora ya kutumika.

Akizungumza leo wakati wa zoezi hilo la ukaguzi lililofanyika wilayani humo, Katibu Tawala alisema kuwa huduma hiyo ni ya kipekee na inadhihirisha dhamira ya kweli ya TEMESA katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja wake, huku akiwasihi viongozi wa TEMESA kuhakikisha huduma hiyo inakuwa ya kudumu na inaingizwa kwenye mfumo.

“tunaipongeza TEMESA, kitendo cha nyinyi kutoka Kwenda kumfwata mteja kunamtambua mteja wako ni nani na inasaidia sana taasisi zetu kujua hali ya magari yatu kwa wakati na kuepuka hitilafu zisizo za lazima. Tunaomba muendelee na huduma hii iingizwe kwenye mfumo ,” alisema Katibu Tawala huyo.

Kwa upande wake, Meneja wa TEMESA Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Maleko, alisema kuwa huduma hiyo imelenga kufanya ukaguzi wa kina wa mifumo yote ya magari inayohusiana na usalama, ikiwa ni pamoja na breki, taa, mfumo wa umeme, na matairi ili kuhakikisha magari yanakidhi viwango vya matumizi salama.

“Hii ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma na kuwasogezea wateja wetu huduma kwa wakati. Tunafanya tathmini ya magari na kutoa mrejesho kwa taasisi husika ili waweze kuchukua hatua stahiki kabla magari hayajapata hitilafu kubwa,” alieleza Eng. Maleko.

Naye Afisa Usafirishaji wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa zoezi hilo limekuwa na manufaa makubwa kwani limewapa nafasi ya kueleza changamoto wanazokumbana nazo kuhusu magari yao, huku wakipata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa TEMESA.

Huduma hiyo inatarajiwa kuimarisha matumizi ya magari ya Serikali kwa usalama, kupunguza gharama za matengenezo makubwa, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.