MKURUGENZI WA HUDUMA SAIDIZI TEMESA AWAAGIZA MAMENEJA KUSHIRIKISHA WATUMISHI WAKATI WA UANDAAJI WA BAJETI

News Image

Posted On: February 10, 2025

Mkurugenzi wa Huduma Saidizi TEMESA Bi. Josephine Matiro amewaagiza Mameneja wa Mikoa na vituo wa Wakala huo kuwashirikisha watumishi waliochini yao katika michakato ya uandaaji wa bajeti ili kuleta chachu ya mabadiliko na manufaa zaidi kwa Wakala.

Akifungua kikao kazi cha utendaji na uandaaji wa bajeti kwa mwaka 2025/26 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TEMESA Makao Makuu Tambukareli jijini dodoma leo, Bi. Matiro amesema kuwa ushirikishwaji wa watumishi kutoka ngazi zote utachangia kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya TEMESA.

Bi Matiro ameongeza kuwa ni muhimu kwa mameneja kuwashirikisha watumishi ili kuchochea fursa kwa watumishi wao kutoa mawazo na michango katika hatua ya kuandaa bajeti ambapo hii itasaidia kuongeza ufanisi wa bajeti, kujenga mazingira ya kazi ya kushirikiana na kuboresha utendaji wa taasisi kwa ujumla.

“Bajeti iwe shirikishi mnapotoka hapa muende mkawashirikishe na wenzenu, yaani bajeti yako iwe inajulikana na watumishi wako ili watumishi walioko kwenye kituo chako waelewe” alisisitiza bi. Matiro.

Aidha ameongeza kuwa, ushirikiano kati ya ngazi zote za uongozi na watumishi unaleta manufaa kwa ajili ya kuimarisha michakato ya kiutendaji katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Bi Matiro amehitimisha kwa kuwataka mameneja kuzingatia matumizi na uwezo wa kituo wakati wa kupanga bajeti zao huku akiwakumbusha kulenga zaidi maslahi ya watumishi ili kuwapa motisha katika utekelezaji wa majukumu ya Wakala.