​DC RUFIJI: TEMESA IFANYE KAZI KWA UAMINIFU NA UFANISI KUONDOA MALALAMIKO

News Image

Posted On: September 23, 2023

Serikali Mkoani Pwani imeutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA ) kufanya majukumu yake kwa uaminifu na kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali ili kuondoa malalamiko kwa wateja . Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, katika kikao cha TEMESA Pwani na wadau, kilichofanyika Kibaha Kwa Mathias, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowelle ameeleza kipindi cha nyuma TEMESA ilinyooshewa vidole kwa gharama kubwa za matengenezo, matengenezo kuchukua muda mrefu na kuchakaa kwa miundombinu.

“Sisi Kama Serikali tunaimani na TEMESA ya sasa kwani tumeona mikakati yao inayolenga kuondoa kero na changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa, tunaimani zile Taasisi na watu ambao waliondoa imani na kukata tamaa watarudi kujionea huduma zilizoboreshwa na kuingia mikataba upya. Tumefurahishwa kwa maboresho mbalimbali, ni imani yangu uboreshaji huo utaleta tija na kutendea haki fedha zinazotengwa na Serikali kuzielekeza TEMESA, “ameeleza Gowelle.

Awali akitoa taarifa fupi ya Wakala huo, Mtendaji Mkuu wa TEMESA Lazaro Kilahala aliishukuru Serikali ya Awamu ya sita na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa TEMESA ili kuweza kutoa huduma bora. Ameeleza kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya shilingi Bilioni 22 zilipokelewa TEMESA kwa ajili ya kazi za karakana, ufundi na vivuko.

“Changamoto kubwa ya awali ni magari kuchelewa TEMESA, tumejitathmini na kugundua tatizo ni mchakato wa ununuzi ambao mlolongo wake ulikuwa mrefu,tumebadili utaratibu, sasa tumeingia mkataba na wazabuni wa vipuri na vilainishi nchini nzima ili kuondoa adha hiyo.”

Kilahala amesema pia wamefunga mfumo wa CCTV Kamera kwenye karakana zote ili kuhakikisha usalama wa vifaa vya wateja ambao kipindi cha nyuma ulilalamikiwa kuwepo mazingira ya udokozi kwa vifaa vyao na sasa utaratibu uliopo ni uwazi, vifaa vinavyofunguliwa vitarudi kwa mteja.

Meneja wa TEMESA Pwani, Mhandisi Rehana Yahaya ameeleza wana wilaya Saba na karakana mbili ambazo zinatoa huduma kwa ukaribu kwa wateja wake. Rehana ameeleza wamejipanga kuboresha huduma zao, kufanya matengenezo kwa wakati na kuboresha huduma za vivuko.

“Kuna changamoto ya kivuko Wilaya ya Mafia, kwasasa kivuko ni kimoja MV. KILINDONI, kinajengwa kingine ili kutoa huduma nzuri na kutatua tatizo la usafiri wa uhakika Mafia ,“amebainisha Rehana.

Mhandisi Hassan Karonda, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA alieleza katika kuboresha huduma zao karakana 13 zinafanyiwa ukarabati nyingine ukarabati zimefikia zaidi ya asilimia 90. Ameeleza pia wametoa mafunzo kwa mafundi wao ili kuendana na teknolojia mpya , ambapo wameshapeleka mafundi 50 Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani