MRADI WA USIMIKAJI WA TAA ZA BARABARA BRT II, KUKUZA UJUZI WA MAFUNDI TEMESA
Posted On: September 09, 2024
Meneja TEMESAKikosi cha Umeme, Mhandisi Pongeza Semakuwa amesema mradi wa usimikaji wa taa za barabarani kwa Barabara za mabasi yaendayo haraka/mwendokasi (BRT phase II) baina ya TEMESA na kampuni ya SINO HYDRO kutoka nchini China umewapa ujuzi na kuwajengea uzoefu mafundi wa TEMESA.
Mhandisi Pongeza ameyasema hayo wakati alipotembelea kukagua maendeleo ya mradi huo eneo la makutano ya Barabara ya Chang’ombe na Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 07 Septemba ambapo TEMESA imeshiriki kusimika taa za barabarani kwenye Barabara za mabasi yaendayo haraka/ mwendokasi 53.
Mhandisi Pongeza amesema ufungaji wa taa hizo upo katika hatua za mwisho za majaribio na makutano yote 53 yameshakamilika pamoja na ufanywaji wa majaribio ya awali ambapo pia amesema mafundi 5 wamejipatia uwezo wa namna ya kuzihudumia taa hizo.
“Makutano yote 53 yameshakamilika, tumeshafunga taa zote na tumeshafanya majaribio ya awali lakini kwa sababu ya kitaalamu majaribio haya inabidi yafanyike kwa siku tano na baadae mradi utakabidhiwa kwa ajili ya matumizi”.
“Tuliamua kushirikiana na wenzetu Sino Hydro ili tuweze kupata ujuzi na kuongeza uzoefu na pindi mradi utakapokabidhiwa Serikalini Wakala utaendelea kuuhudumia tukiwa tunajiamini kwa maana mafundi wetu wameshajifunza na wamepata uelewa mkubwa,” alisisitiza Mhandisi Pongeza.
Halikadhalika Mhandisi Antony Malima ambaye anasimamia usimikaji huo amesema taa hizo ni za kisasa tofauti na zamani ambapo zimeangalia mahitaji ya watu maalumu hasa wasioona.
“Taa hizi zimefungwa mfumo wa sauti ambapo hata mtu asiyeweza kuona ana uwezo wa kusikia sauti ya kumuongoza kukatisha Barabara na viashiria vya wakati ambapo mtumiaji wa Barabara ataweza kutambua muda wa kusimama kwenye baadhi ya makutano ya Barabara”, amesema mhandidi Malima.
Kwa upande mwingine fundi aliyeshiriki kusimika taa hizo amesema kupitia kazi hiyo amejifunza kusimika taa hizo kwa ubora mkubwa na kuahidi kuzihudumia kwa maslahi ya taifa.