WATUMISHI KIKOSI CHA UMEME DAR ES SALAAM WAHIMIZWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA UFANISI
Posted On: June 02, 2025
Watumishi wa Kikosi cha Umeme cha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) jijini Dar es Salaam wamehimizwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, nidhamu na weledi ili kufanikisha malengo ya Taasisi hiyo hususan katika kipindi hiki cha mabadiliko na maboresho ya utendaji kazi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA, Mhandisi Hassan Karonda, wakati wa kikao kazi maalum kilichofanyika katika ofisi za Kikosi hicho, ambapo aliwasisitiza watumishi kuzingatia wajibu wao kikamilifu huku wakijitambua na kuelewa matarajio ya mwajiri wao.
"Kila mmoja anapaswa kuifahamu kazi yake kwa kina, ajitambue na ajue kwa undani matarajio ya mwajiri wake. Hiyo ndiyo njia pekee ya kufanikisha majukumu kwa weledi na ufanisi," alisisitiza Mhandisi Karonda.
Akiweka mkazo zaidi juu ya uadilifu kazini, Mhandisi Karonda alibainisha kuwa utekelezaji bora wa wajibu unahitaji mchanganyiko wa uaminifu, uwajibikaji na nidhamu ya kweli, akisema kuwa hayo ni misingi muhimu inayopaswa kuongoza kila mtumishi wa umma.
"Kutimiza wajibu kazini si suala la hiari; linahitaji mtu kuwa na uaminifu wa ndani na kujituma bila kusukumwa. Hili ndilo changamoto kubwa kwa baadhi ya watumishi, lakini lazima tubadilike," alisema kwa msisitizo.
Kikao kazi hicho kililenga kuongeza morali, mshikamano na uwajibikaji miongoni mwa watumishi, huku kikiwa sehemu ya mikakati ya TEMESA katika kuhakikisha huduma bora, za haraka na zinazokidhi viwango vinatolewa kwa wananchi.
Kwa ujumla, Mkurugenzi Karonda ameonyesha dhamira ya kweli ya kuifikisha TEMESA katika kiwango cha juu cha utoaji huduma bora za kiufundi, akisisitiza kuwa mafanikio hayo hayawezi kufikiwa bila ushirikiano na utayari kutoka kwa kila mtumishi mmoja mmoja.