KIKOSI CHA UMEME KINATEKELEZA MRADI WA BILIONI 12 MJI WA SERIKALI MTUMBA

News Image

Posted On: August 16, 2022

Ofisi ya Kikosi cha Umeme Kanda ya Kati Dodoma inasimamia mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 12 wa kusimika mifumo ya Umeme, Elektroniki, TEHAMA, Viyoyozi, Lifti, Kangavuke pamoja na kamera za usalama katika mji wa Serikali Mtumba mjini Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kikosi cha Umeme Kanda ya Kati Dodoma Mhandisi Deogratius Tarimo wakati akikagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo. Mhandisi Tarimo amesema mradi huo unahusisha jengo la Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ambapo Kikosi cha Umeme kinasimika mifumo ya Umeme, TEHAMA, Lifti na Viyoyozi. Mradi huo kwa jengo hilo unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.1.

Kikosi hicho pia kinasimika mifumo ya Umeme, TEHAMA, na mifumo ya kuzima moto pamoja na Viyoyozi katika jengo jipya linaloendelea kujengwa la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Mhandisi Tarimo amebainisha kua mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.5 kwa upande wa jengo hilo.

Aidha Kikosi cha Umeme Kanda ya Kati Dodoma pia kinatekeleza mradi wa usimikaji wa kamera za usalama katika makutano yote ya barabara zilizoko katika Mji wa Serikali Mtumba, mradi huo una gharimu jumla ya shilingi bilioni 2.5.

Jiwe la Msingi kwa ajili ya ujenzi wa Majengo hayo ya Wizara kwa awamu ya pili ulizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa mnamo Disemba 2, 2021 na miradi yote inatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2024.