UJENZI KIVUKO KIPYA MAFIA NYAMISATI WAFIKIA ASILIMIA 65.3%
Posted On: May 28, 2026
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Lukombe King’ombe tarehe 18 Mei, 2026 amefanya ziara yakutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya cha Mafia Nyamisati ambacho kitakwenda kutoa huduma kati ya Mafia Wilayani Mafia na Nyamisati Wilayani Kibiti Mkoani Pwani.
Kivuko hicho kitakwenda kusaidiana na kivuko MV. KILINDONI ambacho kimeonekana kuzidiwa na wingi wa abiria wanaotumia huduma hiyo na hivyo Serikali kuamua kuongeza kivuko kingine ili kuondoa adha ya usafiri wanayokutana nayo wakazi wa maeneo hayo.
Akizungumza mara baada ya kukagua kivuko hicho eneo la Kimbiji Kigamboni Mkoani Dar es Salaam, Mhandisi King’ombe amesema kuwa Serikali imeamua kuongeza kivuko katika eneo ili kuwanusuru wakazi wa maeneo ya Mafia na Nyamisati ambao mara kwa mara wamekuwa wakilazimika kusubiri kivuko kurudi kutoka upande mwingine zaidi ya siku tatu mpaka nne hivyo kuchelewesha shughuli za maendeleo.
Mhandisi King’ombe amesema kuwa ujenzi wa kivuko hichounaendelea vizuri na kumtaka mkandarasi DMG kuhakikisha anamaliza ujenzi huo kwa haraka ili wakazi wa maeneo hayo wapate usafiri salama na wa uhakika.
“Mpaka sasa tayari ujenzi wa kivuko hiki umefikia asilimia zaidi ya 65.3% na tunatarajia mkandarasi atamaliza ujenzi wa kivuko kwa haraka ili wakazi hawa wapate usafiri wa uhakika.” Amesema Mhandisi King’ombe.
Naye Msimamizi wa mradi kutoka kampuni ya DMG Mhandisi Faustine Simon Lukindo amesema mpaka sasa tayari umbo la kivuko hicho limekwishaanza kuonekana na kazi zinazoendelea ni kukamilisha umbo la nje la meli.
“Kwa sasa tunafanya kazi ya muundo mkuu wa kivuko hiki (Superstructure) ambapo mpaka sasa tumebakiza ngazi mbili ili tuweze kukamilisha umbo la nje la meli, lakini pia kuna kazi ndogo ndogo ambazo zinaendelea kwenye umbo la ndani mfano uwekaji wa mifumo ya mabomba ya kupitisha maji kwakuwa hii ni meli ya abiria, mifumo ya kuzimia moto, mifumo ya kupooza injini, mifumo ya mafuta na mitambo yote ambayo inafanya kivuko kifanye safari zake.” Amesema Mhandisi Faustine.
Kivuko hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa Tani 120, uwezo wa kubeba abiria 300 na magari madogo 10 na ujenzi wake unagharimu shilingi bilioni 9.