UJENZI VIVUKO VIPYA VINNE MWANZA WAFIKIA ASILIMIA 67%
Posted On: October 09, 2023
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) inaendelea na ujenzi wa vivuko vipya vinne Mkoani Mwanza na sasa ujenzi wa vivuko hivyo umefikia asilimia sitini na saba. Ujenzi huo wa vivuko vipya, unafanywa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport Boatyard iliyoko Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza wakisimamiwa kwa karibu na wataalamu kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA).
Vivuko hivyo vinne vinavyojengwa ni pamoja na kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Ijinga na Kahangala Wilayani Magu, kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Bwiro na Bukondo Wilayani Ukerewe, kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Kisorya na Rugezi Wilayani Ukerewe pamoja na kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome Wilayani Sengerema, vyote vikiwa Mkoani Mwanza.
Akizungumza mara baada ya kukagua vivuko hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala huo, Mhandisi Deogratias Nyanda amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 61 kwa ajili ya ujenzi wa vivuko vipya pamoja na ukarabati wa vivuko vinavyoendelea kutoa huduma kote nchini.
‘’Tuko hapa Kanda ya Ziwa kwa ajii ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali iliyotengewa zaidi ya shilingi Bilioni 61, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutenga kiasi hicho cha fedha ambacho kitatuwezesha kufanya ukarabati na ujenzi wa vivuko vipya, ujenzi huu unafanyika ukisimamiwa na mkandarasi wa ndani Songoro Marine ambalo ni wazo zuri sana kwa Seikali yetu kufanya hivi kwasabababu fedha za Serikali zitatumika na zitabaki hapa hapa nchini halikadhalika ubora huu tunaweza tukaukagua sisi wenyewe tofauti na ungefanyikia nje ya nchi, lakini pia gharama zingekua ni kubwa Zaidi.’’ Amesema Mhandisi Nyanda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro, Major Songoro akizungumza mara baada ya ukaguzi huo amesema,kampuni yake inaendelea na ujenzi wa vivuko vipya pamoja na ukarabati wa vivuko vinavyoendelea kutoa huduma, amesema ujenzi wa vivuko hivyo vipya umefikia hatua nzuri na vivuko vyote vinne viko katika hatua ya muundo mkuu (Super Structure).
‘’Tunatarajia kufikia mwisho wa mwaka, kivuko kimoja baada ya kingine vitaanza kuingia kwenye maji ili kuanza majaribio,’’ Amesema Songoro huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na viongozi wengine kwa kuendelea kutoa vipaumbele kwa Kampuni za ndani ambazo kwa kupewa kuteleleza miradi hiyo, zinatoa ajira kwa vijana walioko nchini na hivyo kuleta maendeleo nchini.