MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA UJENZI, UHANDISI, UKANDARASI NA MADINI KUKUZA SEKTA YA UJENZI

News Image

Posted On: December 02, 2024

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mha. Godfrey Kasekenya, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuandaa Maonesho ya teknolojia ya ujenzi ili kuendana na maendeleo ya teknolojia ya kisasa katika kuboresha sekta ya ujenzi, ukandarasi, uhandisi na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kasekenya ameyasema hayo Tarehe 30 Novemba 2024 jijini Dodoma, wakati wa kuhitimisha Maonesho ya Teknolojia ya kisasa katika sekta ya ujenzi, uhandisi, ukandarasi na madini yaliyoandaliwa na kampuni ya Global Expo ltd na kufanyika kwa muda wa siku 10 katika viwanja vya Mashujaa ya zamani relini, ambapo yalivutia washiriki kutoka sekta mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa ikiwemo Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania(TEMESA), Lengo kuu likiwa ni kuimarisha uwekezaji na kukuza sekta ya ujenzi na uhandisi kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazozalisha miradi yenye tija.

Mheshimiwa Kasekenya amewasisitiza waandaaji wa maonesho hayo wahakikishe kuwa wanajitahidi kuendelea kuandaa matamasha na maonesho mengine zaidi ili kuonyesha teknolojia mpya na zenye tija katika sekta ya ujenzi .

"Nikuombe uendelee kuandaa matamasha na maonesho kama haya ambayo ni somo zuri sana kuona, maonesho kama haya ni fursa nzuri kwa sekta mbalimbali kujifunza na kuchangia mawazo mapya, huku tukijizatiti katika kuleta maendeleo endelevu". Alisema Mhandisi Kasekenya.

“Yatakapotokea maonesho mengine kama haya tuendelee kujitokeza kwa wingi na kwakujiandaa vizuri na tuje na vitu vipya zaidi” Alisisitiza.

Aidha, alitoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa za kujifunza na kujua eneo sahihi la kupata wataalamu ,mafunzo na bidhaa bora ili waweze kuijenga Tanzania inayoendana na teknolojia ya kisasa.

“Nitoe rai kwa wananchi, kunapotokea fursa kama hii tusisite kujitokeza na mimi naamini ukuaji wa jiji la dodoma kwa upande wa ujenzi, niwaambie wananchi kwa sasa ndio eneo sahihi kwa kuwekeza, tunatamani kila tunachokiona kinajengwa Dodoma kiwe ni kitu cha kisasa”, alisisitiza.

Aidha, Alimshukuru kila mmoja aliyejumuika katika maonesho hayo na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuendeleza sekta ya ujenzi na uhandisi nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa.