KIGAMBONI KULIPWA FIDIA KWA WATAKAOPISHA UPANUZI WA MAEGESHO YA VIVUKO
Posted On: May 29, 2024
Wizara ya Ujenzi imetenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia wakazi wa Kigamboni watakaopisha eneo la upanuzi wa maegesho ya vivuko.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bungeni jijini Dodoma.
Akizungumzia upande wa maegesho ya vivuko, Bashungwa amesema wizara imeomba kutengewa fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa wakazi wa eneo hilo watakaopisha ujenzi na upanuzi wa maegesho ambapo zoezi la utathmini limekamilika.
Amesema kuwa usimamizi wa mafuta na usimikaji wa mifumo ya kielektroniki unaendelea katika vivuko 19 ambavyo ni MV. KAZI, MV. KIGAMBONI, MV. KILINDONI, MV. MISUNGWI, MV. SENGEREMA, MV. MWANZA, MV. SABASABA, MV. ILEMELA, MV. MARA, MV. CHATO II, MV. TEGEMEO, MV. TEMESA, MV. KOME II, MV. MUSOMA, MV. UJENZI, MV. TANGA, MV. PANGANI II, MV. KILAMBO NA MV. MAFANIKIO.
Aidha, Bashungwa amesema kuwa ujenzi wa maegesho ya Mayenzi – Kanyinya (Ngara) umefikia asilimia 80, Ijinga - Kahangala (Magu) umefikia asilimia 48, Izumacheli (Chato – Nkome) umefikia asilimia 95, Mlimba – Malinyi upande wa Mlimba umefikia asilimia 40 na upande wa Malinyi umefikia asilimia 85 pamoja na maegesho ya Bwiro – Bukondo (Ukerewe).
Kazi nyingine zinazoendelea ni ujenzi wa maegesho 77 katika kituo cha Mwaya – Kajunjumele (Itungi Port) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 95. Hata hivyo, utekelezaji umesimama kutokana na changamoto ya ongezeko la kina cha maji. Mapitio ya usanifu yamefanyika na hivyo ujenzi utaendelea baada ya taratibu za marekebisho ya Mkataba kukamilika.
Bashungwa ameongeza kuwa, mikataba ya ujenzi wa maegesho ya Kisorya – Rugezi, Kahunda – Maisome na Ilunda - Luchelele imesainiwa na ipo katika hatua za awali za kuanza utekelezaji.