​MTENDAJI MKUU TEMESA AWATAKA WAKUU WA VIVUKO KUJITAMBUA KAMA VIONGOZI

News Image

Posted On: April 19, 2024

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala, amewaagiza wakuu wa vivuko vinavyotoa huduma katika Kanda ya Mashariki na Kusini kujitambua kama viongozi na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uweledi mkubwa ili kuleta tija katika utendaji kazi wa vituo wanavyovisimamia.

Mtendaji Mkuu ametoa maagizo hayo leo Tarehe 19 Aprili 2024 wakati wakuu hao wa vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini walipokuwa wakipatiwa semina elekezi kuhusu utekelezaji wa miongozo ya Wakala katika utekelezaji wa majukumu ya uendeshaji wa vivuko kwa minajili ya kutoa huduma bora na yenye tija na ufanisi.

Mtendaji Mkuu amewaeleza wakuu hao wa vivuko kuwa, kiongozi maana yake ni kuwa mtatuzi wa matatizo na wajibu wao wa kwanza kama viongozi ni kusimamia uendeshaji wa vivuko na miundombinu yake, rasilimali zote ikiwemo vivuko, mifumo iliyopo katika vituo, makusanyo ya fedha pamoja na rasilimali watu.

‘’Tunachotaka kuleta kwenu ni mjitambue kama viongozi, kuwa kiongozi maana yake ni kuwa mtatuzi wa matatizo, sio sura yako wala sio urefu wako, suala la kujitambua ni muhimu sana, tusimamie vizuri rasilimali fedha pamoja na rasilimali watu.’’Amesema Kilahala.

Kilahala ameongeza kuwa kwenye eneo la mapato pia kumekuwa na ulegevu na kujisahau katika kukusanya mapato na kuyawasilisha kwa wakati Benki. Amewataka wakuu hao kuzisimamia taratibu za makusanyo ambazo zimewekwa kwenye miongozo na kuwaeleza kuwa zaidi ya onyo, taratibu zitakazofuata kwa atakayekiuka maagizo hayo ni kufikishwa katika vyombo vya sheria na kushitakiwa kwa kutofuata utaratibu wa kukusanya mapato na kuyawasilisha kwa wakati.

‘’Tuko Watanzania karibu milioni 60 mpaka sasa, hebu tujiulizeni Watanzania wangapi wameaminiwa na Serikalihii kupewa kusimamia maliza mabilioni kwa niaba ya Watanzania wengine, lakini hilo halitoshi, wewe ndio umepewa dhamana ya kuvusha wale watu pale, mnavusha watu mamia kwa maelfu pale, maana yake uhai wa wale watu umewekwa mikononi mwako. Nataka kila mmoja wenu ajitambue, kile kivuko unachosimamia pale kina thamani ya mabilioni ya pesa, kwenye jicho la Serikali wewe sio mtu mdogo, wewe ni mtu mkubwa na wa muhimu ndio maana umekabidhiwa vitu hivi vyote hivyo.’’ Amesema Kilahala na kuwataka kuonyesha ukomavu kwa kuaminiwa na Nchi na kusimamia ipaswavyo majukumu na dhamana iliyowekwa kwao.

Wakuu hao wa vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini, wanawakilisha vivuko vinavyotoa huduma katika maeneo ya Magogoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mafia na Nyamisati Mkoani Pwani, Lindi Mjini na Kitunda Mkoani Lindi, Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara, Pangani na Bweni Mkoani Tanga, Utete na Mkongo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.

Chimbuko la kuwepo kwa semina hiyo elekezi kwa wakuu wa vivuko ni maelekezo kutoka kwa Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa aliyoyatoa wakati alipofanya ziara ya kikazi Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani Tarehe 22 Machi, 2024 ambapo alitembelea kivuko cha MV. KILINDONI kinachotoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati na kuagiza semina elekezi zitolewe kwa watumishi waandamizi wa vivuko ili kuondoa uzembe na kero ndogo ndogo zinazojitokeza katika vituo na kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi wanaotumia huduma za vivuko kote Nchini.

Semina hiyo elekezi kwa wakuu wa vivuko inatarajiwa pia kufanyika kwa wakuu wa vivuko Kanda ya Ziwa na Magharibi ambayo inajumuisha vivuko vilivyoko Mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na Mkoa wa Kigoma, ikiwa na lengo la kuwakumbusha kuhusu utunzaji wa vivuko, uzingatiaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayohakikisha uwepo wa usalama wa vivuko, namna bora ya uendeshaji wa vivuko, matengenezo ya vivuko pamoja na mgawanyo wa majukumu kwa watumishi wa kada ya vivuko.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa vivuko TEMESA Mhandisi Sylvester Simfukwe akizungumza wakati akitoa semina hiyo, amesema atahakikisha maagizo yote yaliyotolewa na Mtendaji Mkuu yanawafanya wakuuu hao wa vivuko kujitambua na kuhakikisha magizo hayo yanasimamiwa na yanatekelezwa mara moja ili kubadilisha muenendo wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.