MTENDAJI MKUU TEMESA AWATAKA WATUMISHI KUONGEZA UFANISI KATIKA UTENDAJIKAZI

News Image

Posted On: December 27, 2021

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala leo amefanya ziara ya kukagua utendaji kazi katika vituo vya Wakala huo viliyopo jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni sehemu ya kujionea shughuli za vituo hivyo zinavyoendelea na pia kufahamu vizuri Wakala huo, kujifunza na kuuelewa Wakala zaidi. Akiwa katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu ameongozana na Meneja wa Kikosi cha Umeme Mhandisi Pongeza Semakuwa ambapo alianza kwa kutembelea ofisi za kikosi hicho zilizopo Keko Darajani jijini Da r es Salaam ambapo alipata wasaa wa kuzungumza na menejimenti ya kikosi hicho kabla ya kuzungumza na wafanyakazi ambapo aliwapongeza kwa jitihada wanazozifanya na akawataka wafanyakazi hao kuhakikisha huduma wanazotoa zinaendelea kuwa bora ili kuhakikisha wanafungua fursa za maendeleo kwa Taasisi zingine ambazo wanafanya nazo kazi.

‘’niwapongeze sana sana, mnaonyesha mnafahamu mnachokifanya na jitihada na mipango na mikakati ya kuhakikisha kwamba kinafanyika kwa tija zaidi, hii ni mojawapo ya timu za TEMESA ambayo imejipanga, inafahamu inafanya nini, kwahiyo hongereni sana’’. Alisema Mtendaji Mkuu ambapo aliwapongeza pia watumishi wanaojitolea kwakuwa wangeweza kujitolea mahali popote lakini wamechagua TEMESA hivyo akawapa shukrani za dhati kwa kuwa na moyo wa kujitolea lakini pia akawaahidi kuwa anatumai kadri mambo yanavyozidi kuimarika na hali ikiruhusu watumishi hao wanaweza kufikiriwa kwani nao ni familia ya Wakala huo. Mtendaji Mkuu pia alipata wasaa wa kutembelea mradi wa nyumba za makazi zilizopo magomeni Kota mradi ambao Kikosi cha Umeme kimeshiriki kusimika mifumo ya umeme.

‘’Mimi binafsi lakini pia Serikali kwa ujumla ina matumaini makubwa sana na TEMESA, TEMESA inatazamwa kama kitu kikubwa sana, ina uwezo wa kufanya makubwa zaidi, ya kuwa na tija zaidi, ya kusukuma zaidi maendeleo ya nchi hii kuliko anavyofanya sasa, kwahiyo tunachangamoto ya kuishi mategemeo ya serikali’’, Alimaliza Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa ni wakati sasa wa TEMESA kujitafakari kwenye utendaji wa kila siku na kutatua changamoto hizo.

Aidha Mtendaji Mkuu pia alipata wasaa wa kutembelea kituo cha Wakala wa Ukodishaji Magari (Government Transport Agency GTA) katika ofisi zake zilizopo Keko Darajani ambapo Meneja wa kituo hicho Mhandisi Margareth Julian alimtembeza na akapata wasaa wa kukagua yadi zinazosimamiwa na kituo hicho zilizopo Magomeni Usalama na Temeke jijini Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu alimuagiza meneja wa kituo hicho kuhakikisha anasimamia kwa karibu mikataba ya wapangaji wa yadi zinazomilikiwa na Wakala ili Wakala ufaidike na uwepo wa yadi hizo kama mali ya Taasisi.

Mtendaji Mkuu pia alitembelea kituo cha Magogoni Kigamboni ambapo alizungumza na watumishi na menejimenti ya kituo hicho. Akizungumza katika kikao na watumishi hao Mtendaji Mkuu aliwataka watumishi hao kupokea changamoto wanazozipokea kivukoni hapo na kutengeneza mikakati bora ya kutatua changamoto hizo na malalmiko wanayoyapokea.

‘’Kikubwa ni hicho kwamba japo kutakua na malalamiko, tusirudi nyuma, tusikate tamaa na hata mara moja tusichukie wale wanaotupa yale malalamiko, sikuzote tujue kwamba tuko hapa kuwahudumia na wana haki ya kueleza pale ambapo wanaona wana haki ya kueleza na pale ambapo wanaona kwamba wangestahili zaidi’’, alisema Mtendaji Mkuu ambapo pia alimuagiza Mkuu wa kivuko hicho Mhandisi Samwel Chibwana kuhakikisha wateja wote ambao wanatumia mfumo mpya wa kadi (N-CARD) kurejeshewa pesa zao ambazo zilizonekana kukatwa kimakosa kwenye mifumo baada ya kutokea hitilafu ya kiufundi kwenye kadi zao siku ya Tarehe 21 Disemba, 2021.

Nao mameneja wa vituo hivyo walipata wasaa wa kueleza changamoto ambazo vituo vyao vinakutana nazo katika shughuli zao za kila siku za kiutendaji ambapo Mtendaji Mkuu aliwaahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo na kuzitatua kwa wakati ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa uhakika na ubora uliotukuka.

Mtendaji Mkuu anatarajiwa kuendelea na ziara yake kesho ambapo atatembelea karakana ya MT. Depot iliyopo Keko jijini Dar es Salaam na baadae kumalizia ziara hiyo katika karakana ya Vingunguti.