MTENDAJI MKUU TEMESA AWATAKA WATUMISHI KUONGEZA UZALISHAJI

News Image

Posted On: January 21, 2022

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala amewataka watumishi wa Wakala huo kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi ili kuongeza uzalishaji na kuongeza pato la Wakala huo.

Mtendaji Mkuu ametoa maaagizo hayo wakati wa ziara yake kiutendaji aliyoifanya mwanzoni mwa wiki hii katika Mikoa ya Mwanza, Geita na Mara ambapo ametembelea karakana za mikoa hiyo pamoja na vivuko ambavyo vinatoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo.

Akizungumza na watumishi wa vituo na mikoa hiyo kwa nyakati tofauti, Mtendaji mkuu aliwataka watumishi hao kujiuliza ni namna gani wanaweza kufanya ili kuboresha uzalishaji na kukuza kipato cha vituo vyao.

‘’Tuongeze ufanisi katika maeneo yetu ya kazi ili kuhakikisha tunakua bora zaidi katika utendaji kazi wetu,’’ alisema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa changamoto walizotoa watumishi wa mikoa hiyo zipo na zitaendelea kuwepo hivyo ni jukumu lao pamoja na watumishi wenzao kuhakikisha wanazishinda changamoto hizo na kuboresha uzalishaji wao.

Aidha akiwa katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu pia aliwaagiza mameneja hao kuhakikisha wanafanya maboresho ya namna wanavyokusanya mapato ya vituo vyao na kuondoa dhana ya utegemezi kutoka makao makuu kwani dhana hiyo inawazorotesha kufikia malengo wanayopaswa kuyafikia.

‘’Tujitahidi kuondoa fikra kwamba kuna ruzuku na tujipambanue katika kuhakikisha tunaongeza mapato kwa ajili ya kujiendesha wenyewe, pambaneni kwa taswira hiyo, tujiulize tufanye nini ili kuongeza mapato yetu’’, alisema Mtendaji Mkuu na kuwataka watumishi hao watafakari watakapoondoka TEMESA, watakumbukwa kwa lipi na vizazi vijavyo.

Mtendaji Mkuu alianza alianza ziara hiyo ya kiutendaji kwa kutembelea karakana ya TEMESA Mkoa wa Mwanza, Yadi ya Songoro ambapo alikagua ukarabati wa vivuko vya Wakala huo unaofanywa na kampuni ya Songoro ambapo vivuko vya MV.SABASABA, MV.TEMESA pamoja na MV. MUSOMA vinafanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kufikia muda wake wa ukarabati. Mtendaji Mkuu pia alitembelea kivuko cha MV. KOME II kinachotoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome, aidha alitembelea pia Wilayani Buchosa ambapo amekagua kivuko cha MV.TEGEMEO kinachotoa huduma kati ya Kaunda, kisiwa cha Maisome na Nkome. Kivuko cha MV. TEGEMEO kilifanyiwa ukarabati mkubwa hivi karibuni na kinaendelea vizuri kutoa huduma katika eneo hilo.

Aidha Mtendaji Mkuu pia alitembelea kivuko cha Kigongo Busisi na kukagua vivuko vyote vinavyotoa huduma katika kituo hicho ikiwemo kivuko cha MV. MISUNGWI ambacho kinatarajiwa kuondolewa kwenye maji hivi karibuni kwa ajili ya kupelekwa katika yadi ya Songoro kufanyiwa ukarabati mkubwa, alitembelea kivuko cha MV. CHATO II ambapo pia alikagua ujenzi wa jengo la abiria kupumzikia (Waiting Lounge) linalojengwa katika kituo hicho, alipata pia wasaa wa kukagua maegesho ya kivuko cha MV. TEMESA yaliyopo Luchelele, alitembelea kivuko cha MV. UKARA II kinachotoa huduma kati ya Bugorola na Ukara,

Vilevile alitembelea Mkoani Mara ambapo alikagua karakana ya Mkoa huo, alitembelea kivuko cha MV. UJENZI kinachotoa huduma kati ya Rugezi Wilayani Ukerewe na Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara, pia alikagua kivuko cha MV. CHATO I ambacho kinatoa huduma kati ya Kinesi na Musoma mjini kikiwa ni mbadala wa kivuko cha MV. MUSOMA ambacho kinafanyiwa ukarabati mkubwa katika yadi ya Songoro.

Mtendaji Mkuu alimalizia ziara yake katika kivuko cha MV. ILEMELA kinachotoa huduma kati ya Kayenze, visiwa vya Bezi na Ukerewe ambapo pia alikagua jengo la abiria kivukoni hapo na kuzungumza na watumishi wa kivuko hicho.

Tanzania Census 2022