WAZIRI MKUU APONGEZA MCHANGO WA TEMESA KATIKA KUKUZA MAWASILIANO YAKIMKAKATI
Posted On: March 26, 2026
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amepongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania ( TEMESA) kwa mchango wake katika kuimarisha mawasiliano ya kimkakati yanayofanywa na Maafisa Habari wa Taasisi mbalimbali za Umma.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 25 Machi, 2026 katika ukumbi wa mikutano Ubuntu, Jengo la PAPU jijini Arusha, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 110 wa Wadau wa Utoaji Elimu kwa Umma ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania TBC ambapo TEMESA imeshiriki na Kudhamini mkutano huo uliowakutanisha Maafisa Habari kutoka taasisi mbalimbali za umma pamoja na wadau wa mawasiliano.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa taasisi za umma kushirikiana na vyombo vya habari kufanya mawasiliano ya kimkakati katika kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni Mhe. Christian Makonda ameeleza kuwa Wizara itaendela kushirikiana na wadau mbalimbali, hususan wadau wa kutoa Elimu kwa umma na vyombo vya habari , ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu miradi na maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
TEMESA ni moja ya taasisi za Umma zilizoshiriki mkutano huo ulioanza tarehe 23 Machi na yanatarajiwa kuhimishwa tarehe 27 Machi, 2026.