​MTENDAJI MKUU TEMESA AAGIZA WATUMISHI TEMESA LINDI KUFUATA MIONGOZO

News Image

Posted On: November 09, 2022

Timu ya viongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ikiongozwa na Mtendaji Mkuu Lazaro Kilahala imeendelea na ziara ya kutembelea Ofisi zake kujionea hali halisi na utendaji kazi unavoendelea kwa kutembelea Mkoa wa Lindi, akiwa Mkoani humo, amezungumza na watumishi na kuwakumbusha kufuata miongozo iliyotengenezwa ili kurahisisha na kuleta ufanisi katika kazi kwakuwa miongozo hiyo ndiyo inayopaswa kuwaongoza katika utendaji kazi wao wa kila siku huku akiwasisitizia kubadilisha mitazamo ya namna wanavyofanya kazi ili kuongeza tija na ufanisi.

‘’Tutaibadilisha Lindi kwa kutambua matatizo yetu na kuyatafutia ufumbuzi, tuanze kujifikiria kujiendesha kama Taasisi ya kibiashara na natarajia pale ambapo mmeona patawasaidia ndipo mngeongeza nguvu zaidi ili pawaletee kipato zaidi mfano kwenye matenegenezo ya Viyoyoyozi’’. Amesema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa TEMESA kwa sasa imeboresha na kurahisisha upatikanaji wa vipuri na vilainishi kwa kuingia mikataba ya moja kwa moja na watengenezaji na hiyo imesababisha upatikanaji wake kuwa rahisi na wa bei nafuu kulinganisha na hapo awali hivyo ni wakati sasa watumishi hao wafanye kazi kwa bidi ilikuleta matokeo makubwa katika Taasisi.

Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri Bi. Josephine Matiro akizungumza na watumishi hao amewasisitiza kuimarisha umoja ushirikiano, uwazi na uwajibikaji, kujenga mshikamano, uaminifu na kuzingatia maadili katika utendaji kazi ili kuleta ufanisi. ‘’Kwanza niwapongeze, nafahamu mabadiliko ni hatua lakini tuna hatua nyingine ya kupiga mbele zaidi, turekebishane ili tuweze Kwenda mbele Zaidi, tuweke juhudi Zaidi ili tuongeze kipato chetu, alisema Mkurugenzi Matiro.

Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Hassan Karonda, amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatoa huduma bora za matengenezo ya magari na kuepuka kutoa visingizio na badala yake watengeneze mikakati ya kuboreshautendaji kazi wao kwa manufaa yao na manufaa ya taasisi TEMESA.

‘’Tujue tunachokifanya ili mapato yetu yasogee, Lengo letu tuzalishe, tukishazalisha tukusanye na kuboresha hali zetu’’. Alimaliza Mhandisi Karonda.

Mapema, akisoma taarifa ya utendaji kazi ya Karakana ya Mkoa huo, Meneja wa TEMESA Lindi Mhandisi Rocky Sebigoro amesema kuwa kituo chake kimefanya mkakati wa kuboreshautendaji kazi ikiwemo kupokea mafunzo kutoka kwa Meneja wa TEMESA Dar es Salaam Mhandisi Liberatus Bikulamchi Pamoja na timu yake ambapo miongoni mwa faida walizozipata kutoka kwenye mafunzo hayo ni kupunguza malalamiko kutoka kwa wateja, kuboresha mazingira ya karakana kwa kuondoa uchafu usiotakiwa ikiwemo vyuma chakavu ambapo walipatiwa mafunzo ya KAIZEN. Meneja pia ameongeza kuwa huduma kwa mteja imeimarika baada ya mafunzo hayo baada ya kuanzisha mabalozi ambao wametambulishwa kwa katibu Tawala wa Mkoa huku kazi yao ikiwa ni kuhakikisha Taasisi wanazoziwakilisha zinapatiwa huduma stahiki na zinalipa madeni yao kwa wakati.

Timu hiyo pia ilipata wasaa wa kutembelea na kukagua kivuko cha MV. KITUNDA kinachotoa huduma kati ya Kitunda na Lindi mjini na kuongea na watumishi wanaofanya kazi katika kivuko hicho ambacho kinatarajiwa kupelekwa kwenye matengenezo makubwa hivi karibuni kwakuwa muda wake wa matengenezo tayari umefika.