​BASHUNGWA AITAKA TEMESA KUACHA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA

News Image

Posted On: November 09, 2023

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameuagiza Wakala wa Ufundi na umeme (TEMESA) kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuongeza kasi, weledi naubunifu wa utoaji huduma kwa wadau wake ili kuleta tija kwa Wakala huo. Hayo ameyasema Waziri huyo leo tarehe 08 Novemba, 2023 jijini Dodoma wakati akizindua Bodi ya Ushauri wa Wakala huo ambayo imeundwa na wajumbe Sita kwa Mujibu wa Sheria.

Bashungwa ameutaka Wakala huo kubadilisha mitazamo kwa kuendelea kufanya maboresho kwa watumishi wake na karakana za wilaya na mikoa kwa kuangalia mpango mkakati walioupanga kwa ajili ya kuijenga TEMESA mpya ili kupunguza dhana mbaya ambayo imejengeka kwa jamii dhidi ya Wakala huo.

“Hakikisheni mnabadilisha mitazamo ya kufanya kazi kwa mazoea kwa baadhi ya watumishi, wale ambao bado wapo kwenye kufanya hivi, haya mambo lazima muachane nayo na watakaokuwa wanatuchelewesha msisitite kuwachukulia hatua”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameagiza Wakala huo kuangalia suala la teknolojia kwa huduma wanazozitoa ili kuendana na wakati ikiwemo kuboresha karakana zao kwa kuweka vifaa vya kisasa vinavyoendana na wakati ili kuongeza ufanisi wa Wakala. Ameiagiza Bodi hiyo kukaa na Menejimenti ya Wakala huo kuhakikisha wanaboresha mpango mkakati wao hususan katika suala la ubunifu kwa lengo la kusaidia Wakala huo kubadilika kiutendaji.

Halikadhalika, Waziri Bashungwa ameelekeza Bodi hiyo kuangalia suala la ushirikiano wa kibiashara kati ya Wakala huo na TOYOTA kuona namna ya kulimaliza suala la vipuri bandia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, amesema kuwa Bodi hiyo iliundwa kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha sheria ya Wakala wa Serikali Na. 30 yaa mwaka 1997 na marekebisho yake kupitia sheria Na.13 ya mwaka 2009.

“Bodi hii inaongozwa na Mwenyekiti na wajumbe kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bodi ya Usajili ya Wakandarasi (CRB), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Maendeleo ya Viwanda vidogo (SIDO) pamoja na Shirika la TATC Nyumbu”, amesema Balozi Amour.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Deogratias Nyanda,amemhakikishia Waziri Bashungwa kuwa watatekeleza dhamana waliyopewa kwa uadilifu mkubwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya bodi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuleta tija na ufanisi kwa Wakala huo.