​BASHUNGWA ATOA MIEZI MIWILI TEMESA KUFANYA MAGEUZI

News Image

Posted On: February 05, 2024

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa miezi miwili kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kukamilisha taratibu zote za kiutendaji na Marekebisho ya Kisheria ili kuuwezesha Wakala huo kutekeleza majukumu yake kibiashara ifikapo mwaka mpya wa fedha 2024/25.

Bashungwa amezungumza hayo jijini Dodoma Februari 5, 2024 mara baada ya kupokea wasilisho la Wakala huo ambao unaelezea mkakati wa mabadiliko (Transformation Statergy) na kupata mwarobaini wa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na Wateja kwa Wakala huo.

" Nimefurahishwa na mkakati huu mliouandaa, ni matumaini yangu TEMESA sasa mtabadilika na mtafanya maboresho makubwa katika utoaji wenu wa huduma kama mlivyoeleza", amesema Bashungwa.

Bashungwa ametaka Wakala huo kujikita katika hudoaji wa huduma kwa Watanzania na kuondokana na dhana ya kuweka tozo kubwa ambayo itamnyonya mwananchi kwenye huduma wanazozitoa.

Aidha, Bashungwa ameagiza Wakala huo kukaa mezani na kampuni ya TOYOTA ili kufikia muafaka wa makubaliano ya ununuzi wa vipuri, kubadilishana utaalam na utoaji wa mafunzo kwa wataalam wa TEMESA.

Bashungwa ameeleza kuwa Chimbuko la Mkakati huo limetokana na malalamiko ya wateja kwa TEMESA ikiwemo kutoridhishwa na huduma za Wakala huo katika karakana za Wakala huo ikiwemo uwepo wa vipuri feki, wizi wa vipuri na kuchelewesha huduma kwa wateja wao.

Kadhalika, Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi, Mhandisi Aisha Amour, kuisimamia Timu ya Mkakati wa TEMESA ili kuhakikisha mafunzo kwa mafundi yanapatikana, upatikanaji na uwepo wa vipuri halisi, uwepo wa Software mbalimbali ambazo zinamilikiwa na Serikali, uwepo wa muongozo wa ramani za majengo ya abiria katika vituo vyote nchini pamoja na uwepo wa muongozo wa kutumia ramani moja katika karakana zote nchini.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala, amesema kuwa lengo la kuandaa mkakati huo ni kuendelea kuboresha Wakala huo kupitia huduma zake ambazo unazitoa kwa wateja wake.

Kilahala ametaja mapendekezo yaliyomo kwenye mkakati huo ni pamoja na uboreshaji wa maaeneo ya utoaji huduma ikiwemo karakana, uboreshaji wa maegesho ya abiria, mitambo bora ya kazi na kuwa na huduma nzuri na bora za vivuko kote nchini.