MAAGIZO YA WAZIRI BASHUNGWA MV. KILINDONI YATEKELEZWA

News Image

Posted On: April 02, 2024

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kupitia ofisi yake ya Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini imetekeleza agizo lililotolewa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa alilolitoa Tarehe 22 Machi 2024 wakati alipofanya ziara kukagua utendajikazi wa kivuko MV. KILINDONI kinachotoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati Mkoani Pwani ambapo aliuagiza Wakala kuhakikisha unapeleka vichanja vya kuhifadhia mizigo katika kivuko hicho pamoja na maturubai ili kuhakikisha mizigo na mali za abiria wanaotumia kivuko inakuwa katika hali ya usalama na kuepuka kunyeshewa na mvua.

Akizungumza mara baada ya kutekeleza agizo hilo leo, Meneja wa vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe amesema kuwa, Wakala utaendelea kusimamia usalama wa mali na abiria wake katika maeneo yote ya vivuko nchini na kuhakikisha unawapatia huduma iliyo bora na salama wakati wote.

Mhandisi King’ombe amesema, zoezi hilo litakuwa endelevu kwa kuwa kila wakati wamekuwa wakipeleka vifaa vinavyohitajika katika maeneo mbalimbali ya vivuko vyenye uhitaji ambapo pia amemuelekeza Mkuu wa kivuko kuhakikisha anasimamia vizuri zoezi la upakiaji wa mizigo katika kivuko na kuwasisitiza mabaharia wa kivuko kuzingatia utunzaji wa vifaa hivo katika kivuko.

“Tumeleta vifaa hivyo na ni vitu endelevu ambavyo kila mara tunapaswa kuvileta na tumekuwa tukifanya hivyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Waziri kuwa tutaendelea kutimiza wajibu wetu katika kuyatimiza haya, “ amesema Mhandisi King’ombe.

Mhandisi King’ombe Ameongeza kuwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi, ipo kwenye mkakati wa ujenzi wa kivuko kingine cha pili ambacho kitaongeza kasi ya utoaji huduma na kitapunguza msongamano wa abiria na mizigo na kuchochea hali ya kupakia mizigo kwa kasi na kutakuwa na muda wa kutosha kupangilia mizigo kwenye vivuko.

“Kivuko mnachokiona kimetoka Mafia alfajiri, kimefika hapa majira ya saa mbili na muda wa kupakia unakuwa ni mfupi pamoja na hizi mvua kwa hiyo mara nyingi watu wanaotusaidia kubeba mizigo nao huwa wanapakia kwa haraka hali inayopelekea kuharibika kwa vifaa” amesema Mhandisi Kingombe.

Aidha Mhandisi King’ombe amemhakikishia Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuwa TEMESA itaendela kutimiza wajibu kama alivyoagiza ili wananchi waendelee kupata huduma inayostahili na mizigo yao wanayosafiri nayo itatunzwa vizuri pindi wanaposafiri ili isiharibike.