BASHUNGWA ATOA WITO KWA TEMESA NA ABIRIA KUZINGATIA SHERIA NA USALAMA KWENYE VIVUKO

News Image

Posted On: October 08, 2024

Waziri wa. Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa ametoa wito kwa watumiaji wa Barabara na njia nyingine za usafirishaji hususani vivuko vinavyoendeshwa na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali ya usalama iliyowekwa kwa kuhakikisha hawajai kupita kiasi kwenye vivuko wanapokuwa wanasafiri kwa kutumia usafiri huo na hawazidishi mizigo ili kulinda usalama wao kama abiria pamoja na kulinda mali zao.


Bashungwa ametoa wito huo na maelekezo hayo Mkoani Lindi wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi wakati wa hafla ya uitaji saini miradi dharura ya barabara na madaraja na kutolea mfano ajali iliyotokea Oktoba 03, 2024 Nchini Congo ambapo Meli MV. Merdi ilizama katika Ziwa Kivu na kusababisha vifo na upotevu wa mali.

“Juzi mliona ajali mbaya sana ya kuhuzunisha kwa majirani zetu kule upande Congo ambako meli ilizama na kusababisha vifo vingi sana, kumekuwa na uzidishaji wa mizigo na abiria kinyume cha sheria jambo ambalo linasababisha ajali na kupoteza Maisha ya watu niombe sana kila mmoja wetu awe mlinzi wa mwenzake”,amesema Waziri wa Ujenzi.

“Ni marufuku kwa TEMESA kujaza abiria na mizigo kupita viwango, abiria msikubali kupanda chombo ambacho umeambiwa ujazo umefika ukomo na usiwe mbishi, tunafanya hiyo kwa faida yako kwasababu tunataka tulinde nguvu kazi ya taifa letu kwahiyo nimeona nichukue nafasi hii kutoa maelekezo kwa TEMESA kuzingatia maswala ya usalama kwenye vivuko kwa kuhakikisha hatuzidishi abiria wala mizigo”, amesisitiza Bashungwa.

Aidha Bashungwa amewaasa wananchi kuwa na subra ya kusubiri kivuko kingine pindi wanapoona Kivuko kimejaa ili kuepusha ajali na matukio kama hayo na kuhakikisha wanalinda na kutunza nguvu kazi ya Taifa.