ANDENGENYE AZITAKA TAASISI KIGOMA KULIPIA HUDUMA WANAZOPATA TEMESA KWA WAKATI
Posted On: October 25, 2023
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amezitaka Taasisi zote za Serikali Mkoani Kigoma kuhakikisha zinalipia kwa wakati gharama za huduma zote wanazozipata kutoka karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoani humo ili Wakala huo uweze kutoa huduma endelevu.
Mh. Andengenye ametoa maagizo hayo Tarehe 24 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Kigoma Social Hall wakati alipokuwa akizungumza na wadau wanaopata huduma za matengenezo ya magari, pikipiki, mitambo, TEHAMA, elektroniki na viyoyozi ambao ni Taasisi za Umma na binafsi. Kikao hicho cha wadau kilishirikisha pia washitiri kutoka gereji binafsi, wauzaji wa spea za magari pamoja na vilainishi,
Mkuu wa Mkoa amesema Taasisi hizo kadiri zitakavyokuwa zinalipia huduma kwa wakati ndivyo ambazo zitausaidia Wakala huo kufanya kazi kwa ufanisi.
‘’Kama nilivyosema hapo awali, kwa mwali kuliwe na kwa somo pia kuliwe, tukilipa maana yake tunaijengea uwezo Taasisi yetu kuweza kufanya kazi, nimesema hivyo kwasababu moja ya changamoto iliyopo tunaiunda sisi wenyewe, bahati nzuri mifumo ya Serikali ya sasa hivi inaenda kwa malipo ya papo kwa papo, na tayari fedha za matengenezo ya magari tunayo, sasa tuitumie fedha hiyo kwa ajili ya kufanya malipo ili tusiikate miguu Taasisi ya kwetu TEMESA.’’ Amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Andengenye pia amewaomba wadau pamoja na watawala wa TEMESA kubadilisha fikra zao ili kuisaidia TEMESA kuweza kubadilika kwa kuwa iwapo wao hawatabadilika na TEMESA pia haitaweza kubadilika. ‘’Mabadiliko haya ya TEMESA kama yakienda pasipo sisi wadau kubadilisha na sisi fikra zetu, TEMESA haitaweza kubadilika, tokeni, muende kwenye hizo Taasisi mnazozihudumia mkakutane na Maafisa Usafirishaji, mkakutane na Watawala ili mtengeneze uhusiano wa moja kwa moja wa kutizamana, tunapaswa kujenga uhusiano ambao ni zaidi ya makaratasi ya kuandikiana.’’ Amesema Mhe. Andengenye na kuongeza kuwasisitizia wadau hao kusimamia Maafisa Usafirishaji wao na kulipa kwa wakati madeni lakini pia kuhakikisha wanapeleka magari yao kwa ajili ya matengenezo kinga kwa wakati ili kuepusha magari hayo kuharibika kwa haraka.
Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro N. Kilahala akizungumza katika kikao hicho, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha ili kuboresha miundombinu ya karakana za Wakala ambapo amesema karakana ya Mkoa huo ni miongoni mwa karakana ambazo miundombinu yake inafanyiwa maboresho makubwa kwa sasa ikiwemo ununuzi wa vipuri na ukarabati wa majengo ya karakana ambao unaendelea hivi sasa.
Mmoja wa wadau walioshiriki kikao hicho, Meneja wa Bima ya Afya Mkoa wa Kigoma CPA. Gwamaka Mwakioma akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kikao hicho amesema ameyapokea kwa unyenyekeuvu mabadiliko ambayo Wakala huo umeanza kuyafanya na ana matarajio makubwa ya kuiona TEMESA ikibadilika.
‘’Tunategemea kama kweli yataenda kufanyiwa kazi basi yataboresha maeneo yetu ya kazi na hatutakuwa na changamoto kwenye eneo ambalo wanatuhudumia katika huduma nzima ya utengenezaji wa magari pamoja na vifaa vya umeme pamoja na viyoyozi katika maofisi yetu.’’ Amesema CPA. Mwakioma na kuongeza kuwa wao kama Taasisi wanasubiri kuona utekelezaji ukifanyika ili kuboresha huduma za matengenezo ya magari.