TEMESA YAOMBA RADHI KUFUATIA KUSIMAMA KUTOA HUDUMA KWA MV.KAZI

News Image

Posted On: February 05, 2022

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala leo ametembelea na kukagua Kivuko cha MV.Kazi ambacho kilishindwa kutoa huduma kwa siku nzima ya jana kufuatia kupata hitilafu ambayo ilitokea majira ya asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua Kivuko hicho, Mtendaji Mkuu Kilahala amesema kulitokea hitilafu ambayo ilisababisha kusimama kwa kivuko hicho ili kiweze kufanyiwa marekebisho ambayo yalichukua siku nzima kukamilika na hivyo kusababisha adha kubwa kwa abiria ambao wanategemea kivuko hicho.

Aidha Mtendaji Mkuu pia, alitumia fursa hiyo kuwaomba radhi abiria wanaotumia kivuko hicho kufuatia kukosa huduma ya kivuko cha MV. KAZI kwa siku nzima ambapo alisisitiza kwamba TEMESA inajali usalama wa watumiaji wa kivuko na ndio sababu waliamua kusitisha huduma za kivuko hicho ili kulinda usalama wa abiria na mali zao.

‘’Kama mtoa huduma, tunatumia fursa hii kuwaomba radhi wateja wetu kwa usumbufu ambao umejitokeza jana, pia tutumie fursa hii kuwaeleza wananchi wetu na watumiaji wetu wa vivuko kwamba TEMESA kama Wakala tumejipanga kuhakikisha wakati wote matengenezo yanafanyika kwenye hivi vivuko, Serikali inalipa jambo la usalama kipaumbele cha hali ya juu mno, usalama wa vivuko, usalama wenu ni kipaumbele cha Serikali ''. Alisema Mtendaji Mkuu.

Aidha Mtendaji Mkuu alisema kuwa Serikali imeshatenga fedha za kutosha kuhakikisha vivuko vyote vinafanyiwa matengenezo makubwa na kwa wakati na hivi karibuni kivuko cha MV Kazi kitatolewa majini ili kwenda kufanyiwa matengenezo makubwa kwakuwa kimefikia muda wa matengenezo. Ameongeza kuwa Serikali tayari imekwishatenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa kivuko kingine cha nne ambacho kitakwenda kuondoa adha ya foleni katika kivuko cha Magogoni Kigamboni.

‘’Kama mtakumbuka, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alitoa ahadi kwamba atatuongezea hapa kivuko cha nne baada ya kuiona adha ambayo wananchi wa hapa mnaipata, niwahakikishie kwamba lile agizo tayari limekwishafanyiwa kazi na ununuzi wa kivuko cha nne tayari umekwishaingia kwenye bajeti ya mwakani kwahiyo kuanzia mwezi Julai 2022 tunaanza kujenga kivuko cha nne’’. Alimaliza Mtendaji mkuu na kusisitiza kuwa changamoto za usafiri sasa zinakwenda kupungua katika kivuko hicho.

Mtendaji Mkuu alimaliza kwa kuwashukuru wananchi wanaotumia huduma za kivuko hicho kwa kuendelea kutumia huduma za TEMESA na kuwaahidi kwamba huduma zitaendelea kuboreshwa katika vivuko vyote nchini na hali ya usalama wa abiria na malizao itaendelea kuwa kipaumbele kwa upande wa Serikali.

Kwa upande wa abiria wanaotumia kivuko cha Magogoni Kigamboni, wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma katika kivuko hicho.