AJALI YA BUS KUZAMA KATIKA ENEO LA KIVUKO CHA PANGANI BWENI
Posted On: July 24, 2023
Siku ya Jumapili, Tarehe 23/07/2023 majira ya saa sita za mchana, kumetokea ajali katika eneo la Pangani ambapo kivuko cha MV. TANGA na MV. PANGANI II vinatoa huduma kati ya Pangani na Bweni Wilayani Pangani Mkoani Tanga baada ya Basi la abiria linalotambulika kwa jina la MOA linalofanya safari zake kutoka Tanga mjini kupitia Pangani na kuvuka kwenye kivuko hadi Kipumbwi kuzama baada ya kufika upande wa Bweni lilipokuwa likivuka kutokea upande wa Pangani Kuelekea Bweni.
Akizungumza eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi. Zainab Abdallah ambaye alifika eneo la tukio mara baada ya ajali hiyo kutokea, amesema kuwa hakuna yeyote aliyepoteza maisha wala majeruhi kwenye ajali husika kwakuwa Basi hilo lilikwisha toka kwenye eneo la kivuko na kwa bahati mbaya lilizimika likiwa nje ya gati, dereva alijitahidi kuliwasha tena ili kuliondoa lakini alishindwa kulimudu kwakuwa eneo hilo ni la muinuko na Basi hilo kurudi kinyume nyume na kutumbukia kwenye maji. Dereva wa Basi hilo aliruka na kujiokoa.
''Basi la Kampuni ya MOA ambalo leo (Jumapili) lilitumbukia majini likiwa linatoka ndani ya kivuko kwenda nchi kavu Pangani tayari limetolewa kwenye maji, nawapa pole wana Pangani na Watanzania kwa taharuki na tunafuatilia ili matukio kama haya yasijirudie tena.'' Amesema Bi Zainab.
Hakukuwa na majeruhi yoyote aliyeripotiwa kutoka kwenye ajali hiyo kwakuwa abiria wote walikuwa tayari wameshushwa kutoka kwenye Basi husika kama ambavyo sheria za usalama wa vivuko zinaagiza, vilevile abiria huanza kushuka kwanza kutoka kwenye kivuko kabla ya magari kuruhusiwa kuanza kutoka.
Aidha hadi hivi sasa, shughuli za uvushaji katika eneo hilo zinaendelea kama kawaida na Vyombo vya Usalama tayari vimefanikiwa kuliopoa Basi hilo kutoka kwenye maji kwa kusaidiana na wakandarasi wanaotengeneza daraja la Mto Pangani.
TEMESA inaendelea kuwasisitizia abiria kufuata maelekezo ya usalama yanayotolewa na mabaharia wakati wote wanapotumia vivuko na inatoa pole kwa wahusika wa Basi lililopata ajali lakini pia inawakumbusha wamiliki wa magari kuhakikisha magari yao yanakua katika hali bora wakati wote ili kuepusha ajali zinazoepukika.