MIRADI YA BILIONI 82 YAENDELEA KUTEKELEZWA NA TEMESA, MIAKA MITATU YA RAIS SAMIA

News Image

Posted On: April 08, 2024

TEMESA wamekua mashuhuda wa nia ya dhati ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanatatua changamoto zote zinazokwaza wananchi kufikia malengo yao ya kiuchumi na kijamii.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TEMESA Lazaro Kilahala wakati akitoa wasilisho la mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa TEMESA, lilioandaliwa na Wizara ya Ujenzi na kufanyika siku ya Tarehe 5 Aprili 2024, katika ukumbi wa Mabeyo Complex ulioko mjini Dodoma.

Kilahala amesema katika Miaka Mitatu ya Dkt. Samia Suluhu madarakani TEMESA imeanzisha na imeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya vivuko yenye Thamani ya shilingi bilioni 82.

“Katika miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu tangu ameingia madarakani, TEMESA imeanzisha na inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya vivuko ambayo inathamani ya shilingi bilioni 82, hii hata kwa historia ya TEMESA ni kitu cha tofauti kuwahi kutokea.”

Kilahala amesema kati ya shilingi bilioni 82 asilimia 90 ya kazi zinafanywa na wakandaradi wazawa ambapo shilingi bilioni 42 zimeelekezwa kujenga vivuko vipya ambavyo vitaenda kutoa huduma kwenye maeneo ambayo wananchi walikua wanatumia mitumbwi kuvuka na maeneo mengine ambayo yalikua yamekosa kabisa huduma za vivuko.

Kilahala ameyataja baadhi ya maeneo ambayo hayana huduma za vivuko ikiwemo Ijinga - Kihangala, Bwiro-Bukondo, Buyagu - Mbalika ambapo ndani ya miaka mitatu vivuko vimeendelea kujengwa na ujenzi umefikia asilimia 80.