DENI LA BIL 7/- LAKWAMISHA UKAMILISHAJI UJENZI WA VIVUKO

News Image

Posted On: March 28, 2024

Kamati ya Kudumu ya Bunge Miundombinu imeiagiza Serikali kumlipa mkandarasi Songoro Marine Transport LTD sh. Bilioni 7 anazodai ili akamilishe ujenzi wa vivuko.

Akizungumza Juzi baada ya kamati hiyo kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na mkandarasi huyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Kakoso alisema wananchi wengi Kanda ya Ziwa wanauhitaji wa vivuko hivyo.

Hivyo, alimuagiza Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuhakikisha anapeleka fedha hizo kwenye huo mradi ili uweze kukamilika kwa wakati na kutorudisha nyuma makandarasi wazawa katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Hapa ingekuwa mkandarasi kutoka nje ya nchi mngemlipa riba lakini kwa kuwa ni mkandarasi mzawa bado nayeye anahitaji kuendelea kukua ataishi kwa maumivu makali anaogopa akidai kwa kulazimisha mtamnyima tenda, ndicho kinachowaua wazawa”, alisema Kakoso.

Baada ya maagizo hayo Waziri Bashungwa aliahidi kufuatilia suala hilo baada ya ziara hiyo ambapo alisema ataenda kuweka kambi hazina kwa ajili ya kumuomba Waziri wa Fedha na wataalamu wake kulizingatia hitaji kubwa la mkandarasi huyo kulipwa fedha hizo ili wananchi waweze kupata huduma baada ya miradi hiyo kukamilika.

Mtendaji Mkuu Lazaro Kilahala akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa kivuko kipya na maegesho ya Buyagu-Mbalika alisema kivuko hicho chenye urefu wa mita 30.25, upana mita 9.75 kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 50, abiria 100 na magari madogo sita.

Alisema mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 45.9 na umeongezwa muda kwa miezi minne bila ongezeko la gharama kutokana na kuchelewa kwa malipo baada ya kuwasilisha hati za madai.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Transport, Major Songoro alisema tatizo walilokutana nalo ni kuchelewa kwa malipo ambapo mpaka sasa ni zaidi ya shilingi bilioni saba.

“Katika karakana yetu ya Mwanza tunatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Rugezi-Kisorya ambao umefikia asilimia 81,Ijinga –Kahangala asilimia 84,Bwiro –Bukondo asilimia 85,Nyakalilo – Kome asilimia 60 na Buyagu _ mablika asilimia 45.9”, alisema Songoro.