MAKALA YA MIAKA 62 YA UHURU: MABORESHO MAKUBWA YANAYOENDA KUIBADILISHA TEMESA
Posted On: December 18, 2023
Katika kusherehekea Miaka Sitini na Mbili ya Uhuru, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imeendelea kuboresha huduma zinazotolewa na Wakala huo kuanzia kwenye huduma za usafiri wa kwenye maji pamoja na maboresho katika karakana ili kuhakikisha Wakala huo unatoa huduma iliyo bora ya uhakika na yenye tija kwa Watanzania.
Kabla ya Uhuru na baada ya Uhuru, maeneo mengi ya Nchi ambayo yamezungukwa na maji na Visiwa, yalikuwa hayana usafiri wa uhakika na hivyo wananchi wengi wa maeneo hayo walijikuta wakitumia aina za usafiri ambao sio salama kwa watumiaji kama vile mitumbwi midogo ya mbao ambayo wakati fulani iligharimu maisha ya watu pamoja na mali zao kwa kuzama.
Katika kutekeleza adhma ya kutoa huduma bora kwa wananchi wake upande wa huduma za vivuko, ndani ya Miaka Sitini na Mbili ya Uhuru, Wakala umeendelea kuboresha na kusimamia uendeshaji wa vivuko vya Serikali kote Nchini kwa kuendelea kuongeza idadi ya vivuko, wakati Wakala unaanzishwa mwaka 2005 kulikuwa na jumla ya ya vivuko 13 pekee, Serikali imeuwezesha Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), kuongeza idadi hiyo na mpaka wakati huu Wakala unaendesha jumla ya vivuko 32 katika vituo 22 kote nchini vinavyosimamiwa kupitia Ofisi za Kanda za Mashariki na Kusini na Kanda ya Ziwa na Magharibi. Hii yote ikiwa ni kwa ajili ya kuwahakikishia Watanzania wanaoishi maeneo ya nchi yaliyozungukwa na maji wanafanya shughuli zao za Kiuchumi bila mkwamo.
Tangu Uhuru mpaka sasa, Serikali imeweza kujenga Vivuko vipya kadha wa kadha katika maeneo mbalimbali Nchini ili kuwasaidia Wananchi katika eneo la usafiri wa maji ikiwemo kivuko MV.KAZI, MV. MWANZA, MV, ILEMELA, MV, UKARA, MV.CHATO II, pamoja na MV, KILINDONI. Vivuko vipya vinne vinaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali Nchini ikiwemo kivuko kitakachokwenda kutoa huduma maeneo ya Kisorya na Rugezi, Ijinga na Kahangala, Nyakarilo na Kome pamoja na Bwiro na Bukondo na kwa wastani, ujenzi wa vivuko vyote vinne umefikia zaidi ya Asilimia 70%.
Aidha, eneo la Buyagu na Mbalika, Serikali kupitia TEMESA tayari imesaini mkataba wa kuanza ujenzi wa kivuko kipya huku vivuko vingine vikiwa katika hatua za mwisho za utekelezaji wa mikataba kabla ya kuanza kwa ujenzi wake ambavyo vitakwenda kutoa huduma maeneo ya Mafia na Nyamisati na Magogoni Kigamboni ambako kutajengwa vivuko vidogo viwili (Sea Taxi). Ujenzi wa vivuko hivi vipya unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi na mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka 2024 na unatarajiwa kwenda kuondoa kwa kiasi kikubwa adha ya usafiri inayowakabili wakazi wa Mikoa husika ambao wengi wao wanaishi katika Visiwa viliyopo kando kando ya Ziwa, bahari na Mito na hutegemea shughuli za uvuvi. Ujenzi wa vivuko vyote hivyo unagharimu jumla ya shilingi Bilioni 42 ambazo zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha huduma ya vivuko kwa wananchi.
Sambamba na miradi ya ujenzi wa vivuko vipya, ndani ya Miaka Sitini na Mbili ya Uhuru, Serikali kupitia TEMESA pia inalo jukumu la kuhakikisha vivuko vinavyoendelea kutoa huduma vinakuwa bora na salama wakati wote kwa ajili ya matumizi. Wakala umeweza kukamilisha ukarabati mkubwa wa vivuko vya MV. KAZI, MV. MUSOMA, MV. MISUNGWI, MV. TANGA, MV. TEMESA, MV. MARA NA MV. UJENZI. Aidha, Wakala pia unaendelea na ukarabati wa vivuko tisa ambavyo ni MV. MAGOGONI, MV. NYERERE, MV. KILOMBERO II, MV. KITUNDA, MV. KYANYABASA, MV. RUHUHU, MV. OLD RUVUVU NA MV. MKONGO.
Pamoja na ujenzi wa vivuko vipya, Serikali Kupitia TEMESA pia imeendelea kufanya maboresho katika miundombinu ya vivuko katika maeneo mbalimbali hapa Nchini, imeweza kutekeleza miradi tisa ya ujenzi na ukarabati wa maegesho ya vivuko ambayo ni Izumacheli, Nkome, Chato, Mayenzi-Kanyinya, Ijinga-Kaghangala, Bwiro-Bukondo, Kikove-Ngoheranga, Kanjunjumele-Mwaya na Iramba-Majita. Upande wa Ujenzi wa Miundombinu, ulitekeleza jumla ya miradi mitatu ya ujenzi na ukarabati wa Miundombinu ya Majengo ya Abiria, Ofisi, Vyoo na Uzio ya vivuko ambayo ni Chato, Mwigobero na Lugasa.
Kwa Upande wa Karakana, Miaka Sitini na Mbili ya Uhuru, Serikali imeuwezesha Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kufungua karakana katika Mikoa yote26 upande wa Tanzania Bara pamoja na karakana za Wilaya ambazo zimeanzishwa zikiwa na lengo la kusogeza karibu huduma hiyo kwa Taasisi na Ofisi za Halmashauri ambazo zipo mbali na karakana za Mikoa husika.
- Serikali kupitia TEMESA imeweza kutoa zaidi ya shilingi Bilioni 7.2 ambazo zimewezesha ujenzi wa karakana mpya katika Mkoa wa Simiyu pamoja na kutekeleza miradi ya ukarabati wa Karakana sita za mikoa ya Mwanza, Arusha, Mtwara, Tabora, Kigoma na Mara. Aidha, katika kipindi cha miaka minne, Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 1.1 kwa ajili ya kununua vitendea kazi vipya ambavyo vinatumika katika karakana za Wakala kote nchini upande wa umeme, viyoyozi, majokofu na TEHAMA na kila mwaka imekuwa ikifanya hivyo ili kuhakikisha TEMESA inapata vitendea kazi vya kisasa na kuweza kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ambayo yanaendelea kujitokeza katika magari mapya yanayoendelea kutengenezwa.
- Miaka Sitini na Mbili ya Uhuru pia inaenda na mabadiliko ya Kiteknolojia na Wakala haujakaa mbali na suala la Teknolojia, Wakala umeweza kutekeleza na unaendelea kutekeleza miradi ya Usimikaji wa Mifumo ya Kielekroniki katika ofisi zake kote nchi pamoja na vituo vya uzalishaji ikiwemo Mfumo wa kusimamia mapato yanayokusanywa kwa kutumia POS, Mfumo wa kusimamia matumizi ya mafuta katika Vivuko, Kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato Kigongo-Busisi, Mfumo wa ERMS pamoja na mfumo wa kusimamia Matengenezo ya Magari.
- Wakala unatekeleza miradi hiyo ya usimikaji wa mifumo ya kielektroniki kwa lengo la kuboresha Utendaji kazi wa Wakala
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA Lazaro N. Kilahala anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa ruzuku kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na maelekezo ya kuimarisha utendaji wa Wakala pamoja na kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika eneo la ujenzi wa vivuko vipya pamoja na ujenzi wa karakana mpya na maboresho ya karakana zilizopo ili kuhakikisha maisha ya Mtanzania yanazidi kuimarika kiuchumi siku hadi siku huku akijivunia mafanikio ambayo TEMESA imeweza kuyafikia ndani ya Miaka Sitini na Mbili ya Uhuru.
Aidha, anaahidi uwekezaji huu wa Serikali utatunzwa huku Wakala ukiendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo na ushauri ili kuendelea kuboresha huduma zake.
Baada ya Miaka Sitini na Mbili ya Uhuru, hivi ndivyo Serikali ya Awamu ya Sita inavyoendelea kutekeleza kwa vitendo mahitaji ya Wananchi ili kuboresha hali zao za kiuchumi kwa kuwajengea vivuko vipya na vya kisasa pamoja na kuwaboreshea huduma za karakana.