KONGAMANO LA 10 LA UNUNUZI WA UMMA 2026 LAFUNGWA RASMI ARUSHA

News Image

Posted On: July 31, 2026

Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma la Mwaka 2026 limefungwa rasmi leo, Julai 31, 2026, jijini Arusha na Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mha. Mshamu Ali Munde, baada ya siku tatu za mijadala, mawasilisho na kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuendelea kuimarisha mfumo wa ununuzi wa umma nchini.

Kongamano hilo limewakutanisha taasisi za umma, sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na wataalamu wa ununuzi na ugavi, likiwa jukwaa la kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji, matumizi bora ya rasilimali za umma na kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma.

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki kongamano hilo kwa kudhamini na kutoa elimu kuhusu utoaji huduma kidijitali hususan katika mfumo wa manunuzi ambao upo katika hatua za kutangamanishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Manunuzi wa TEMESA, (MUM).

Aidha, ushiriki wa TEMESA umeendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano na wadau mbalimbali wa Sekta ya umma na binafsi, sambamba na kutangaza uwezo wa Wakala katika kutoa huduma bora za kiufundi zinazochangia maendeleo ya uchumi na utoaji wa huduma kwa wananchi kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.