​TEMESA YAPOKEA CHETI CHA USHIRIKI KATIKA KONGAMANO LA KUMI LA UNUNUZI WA UMMA 2026 ARUSHA

News Image

Posted On: July 30, 2026

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umepokea cheti cha ushiriki katika Kongamano la Kumi la Ununuzi wa Umma la Mwaka 2026 na utambuzi wa mchango wa Wakala. Kongamano hilo la siku tatu linafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC), kilichopo jijini Arusha.

Kongamano hilo lenye kaulimbiu isemayo, "Kutumia Fursa za Ununuzi wa Umma Kidijitali Kufikia Uchumi Endelevu, Jumuishi na Shindani kuelekea Dira ya Taifa 2050," limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya ununuzi wa Umma kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kuimarisha uwazi, ufanisi na tija katika mifumo ya ununuzi wa Umma.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu Mhandisi Pongeza Semakuwa mara baada ya kupokea cheti, amesema ushiriki huu ni fursa nzuri ya kutoa elimu hasa katika mabadiliko ya kidigitali.

“Tumeshiriki maonesho na kongamano hili ili kuwafikia wadau wote na watumiaji wa Mfumo wa NeST ili kutoa elimu ya mifumo kutokana na kwamba tumetangamanisha hii mifumo miwili NeST na Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM), ambapo ikianza kufanya kazi, mtumiaji ataweza kuomba huduma za matengenezo TEMESA kwa kutumia Mfumo wa Manunuzi (NeST)” amesema Mha. Pongeza.

Kongamano hilo la kumi lenye kauli mbiu “Kutumia Fursa za Ununuzi wa Umma Kidijitali, Kufikia Uchumi Endelevu, Jumuishi na Shindani kuelekea Dira ya Taifa 2050”, limefunguliwa rasmi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila.