MAKAMU WA RAIS AWEKA JIWE LA MSINGI KIWANDA CHA KUTENGENEZA MIPIRA YA MIKONO (GLOVES) IDOFI AMBACHO TEMESA IMESHIRIKI KUSIMIKA MIFUMO YA UMEME

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali itaendelea kuchagiza uwekezaji kwenye maeneo yote ya huduma za afya kuanzia ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa vifaa tiba, wataalam pamoja na ujenzi wa viwanda vya bidhaa za afya. Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha mipira ya mikono (Gloves) kinachosimamiwa na Bohari ya Dawa (MSD) kilichopo Idofi , Makambako mkoani Njombe. Amesema Dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. ni kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii kwa kuimarisha afya na kuwezesha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo. Itakumbukwa kwamba, Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kupitia Kikosi cha Umeme ulishiriki kazi ya kusimika mifumo ya Umeme katika kiwanda hicho kipya cha Bohari ya Madawa nchini MSD kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa ujenzi wake na Kikosi hicho kiliweza kusimika mifumo hiyo ya umeme kuanzia kwenye transfoma mpaka ndani. Makamu wa Rais amesema serikali itahakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi kwa ufanisi kwa kuzingatia faida zake kwa taifa ikiwemo kuongeza upatikanaji wa mipira ya mikono (gloves), kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kupunguza muda mrefu unaotumika katika kuagiza bidhaa hizi kutoka nje ya nchi. Amesema kwa sasa Serikali kwa kupitia MSD inaagiza kutoka nchi mbalimbali duniani, 80% ya dawa, 90% ya vifaa tiba na 100% ya vitendanishi.