MKUU WA MKOA WA KATAVI AZIAGIZA TAASISI MKOANI HUMO KULIPIA HUDUMA WANAZOPATIWA NA TEMESA KWA WAKATI.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwamvua Mrindoko ameziagiza Taasisi zote za Umma zilizopo Mkoani Katavi kuhakikisha wanalipia huduma wanazopatiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa wakati ili kuuwezesha Wakala huo kufanya kazi zake kwa ufanisi. Mhe. Mrindoko, ameyasema hayo leo Alhamisi, Tarehe 26 Oktoba, 2023 alipokuwa akifungua kikao cha wadau wanaotumia huduma za TEMESA kwa Mkoa wa Katavi katika ukumbi wa Katavi Resort ulioko Mkoani humo. Mkuu wa Mkoa pia ameupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA)kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ikiwemo ujenzi wa karakana mpya katika Mikoa mbalimbali, ununuzi wa vitendea kazi vya karakana na kazi za umeme pamoja na ukarabati wa karakana zilizochakaa yote ikiwa ni kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi. Aidha, amewaagiza watendaji wa Wakala kufanya kazi kwa ufanisi na weledi mkubwa ili kuwaridhisha wateja wanaotumia huduma za Wakala.