UJENZI VIVUKO VIPYA VINNE MWANZA WAFIKIA ASILIMIA 60%

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala, mwishoni mwa wiki hii ametembelea Yadi ya Songoro iliyoko Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza kukagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko vipya vinne na ukarabati wa vivuko unaoendelea Mkoani humo. Vivuko hivyo vinne vinavyojengwa ni pamoja na kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Ijinga na Kahangala Wilayani Magu, kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Bwiro na Bukondo Wilayani Ukerewe, kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Kisorya na Rugezi Wilayani Ukerewe pamoja na kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome Wilayani Sengerema, vyote vikiwa Mkoani Mwanza.