SERIKALI YASAINI MKATABA WA BILIONI 3.8 KUJENGA KIVUKO KIPYA BUYAGU MBALIKA

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), leo Tarehe 23 Aprili, 2023 imesaini Mkataba wa ujenzi wa kivuko kipya kitakachogharimu shilingi Bilioni 3.8 mpaka kukamilika kwa ajili ya kutoa huduma katika maeneo ya Buyagu na Mbalika Wilaya za Sengerema na Misungwi Mkoani Mwanza. Hafla ya utiaji saini mkataba huo ambao Serikali imesaini na Kampuni ya Kizalendo ya Songoro Marine Transport Limited ya jijini Mwanza, imefanyika katika viwanja vya Sabasaba Wilayani Sengerema na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya ambaye alikua mgeni rasmi.