MTENDAJI MKUU TEMESA AKAGUA UKARABATI KIVUKO CHA MV.TANGA
Mtendaji Mkuu TEMESA Lazaro N. Kilahala, leo amekagua ukarabati unaoendelea wa kivuko cha MV.TANGA kinachofanyiwa ukarabati mkubwa katika eneo la Pangani Mkoani Tanga na kumuagiza mkandarasi kuhakikisha anamaliza ukarabati huo haraka iwezekanavyo ili kivuko hicho kirejee kutoa huduma katika eneo hilo ambapo mkandarasi, Kampuni ya DMG aliahidi kumaliza ukarabati huo ndani ya mwezi huu wa Novemba. Awali Mtendaji Mkuu alitembelea karakana ya Mkoa wa Tanga na kuzungumza na watumishi ambapo aliwaagiza kubadili namna wanavyofikiri kwani miongoni mwa mabadiliko makubwa kabisa yanayotakiwa kutokea TEMESA, badiliko kubwa ni namna ya kufikiri kibiashara zaidi. Kilahala amesema sehemu kubwa ya tatizo la TEMESA ilikuwa ni kutokutambua kwamba kuna tatizo hivyo akaupongeza uongozi wa Mkoa huo chini ya Meneja wa Mkoa Mhandisi Jairos Nkoroka kwa kutambua kwamba kuna tatizo na kuonyesha ari ya kutatua matatizo yaliyopo huku akiwasisitizia kubadili mitazamo ya utendaji kazi na kutatua yale ambayo yamekuwa yakilalamikiwa siku zote. ''Niwape changamoto menejimenti yenu, mjielekeze katika namna gani kituo chenu kitaweza kujiendesha na kuwa kituo cha biashara ambacho kipo kibiashara zaidi na kinatengeneza mapato yake ya kukiwezesha kujitegemea.''