TEMESA KILIMANJARO YASIMIKA MIFUMO JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA MAWENZI

Ofisi ya Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Mkoa wa Kilimanjaro imeshiriki katika mradi wa kusimika mifumo ya Umeme, Elektroniki, Viyoyozi, Viashiria moto (Fire Alarm), (medical gas), TEHAMA pamoja na kubuni na kusimamia kusimika mifumo ya lifti katika jengo la Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Mawenzi iliyoko Mkoani Kilimanjaro. Jengo hilo la hospitali ujenzi wake ulianza Tarehe 15 mwezi Oktoba mwaka 2021 huku jiwe la msingi likiwekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Meneja wa TEMESA Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Sunday Kyungai ameushukuru uongozi wa Wizara ya Afya kwa kuuamini Wakala na kuupatia usimamizi wa mradi huo mkubwa na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi ili kuboresha miundombinu ya majengo ya Serikali Mkoani Kilimanjaro. Ujenzi wa Jengo hilo la Afya ya Mama na Mtoto unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.