TEMESA VINGUNGUTI YAFANYA UTALII WA NDANI ZANZIBAR
Mojawapo ya juhudi kubwa ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya ili kuhakikisha inakuza desturi ya Watanzania kutangaza na kutembelea vivutio vyake vya Kiutalii ni kuhamasisha utamaduni wa kufanya utalii wa ndani kwa watanzania walio wengi ili kukuza pato la taifa. Watumishi wa wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA katika kukuza tamaduni hiyo, mwishoni mwa wiki iliyopita wamefanya ziara ya kitalii katika Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Jozani Chwaka bay unaopatikana Visiwani Zanzibar. Msitu huo unasifika kwa kuwa na miti mirefu, ndege na nyani wekundu maarufu kama ‘Red Colobus’ ambao wanapatikana kwa wingi ndani ya Hifadhi hiyo. Hifadhi ya Jozani Chwaka Bay ina urefu wa kilometa 50 na Eneo la Mraba mita 19 na ndani yake wanapatikana pia ndege zaidi ya aina 40, vipepeo zaidi ya aina 50 pamoja na wanyama wengine mbalimbali. Ndani ya hifadhi hiyo pia, kunapatikana miti mbalimbali ikiwemo miti ya kutengenezea dawa za asili pamoja na miti ya Mikoko ambayo imetapakaa kando ya ufuo wa Kusini. Inakadiriwa kwamba Hifadhi hiyo hutembelewa na karibu asilimia 10 ya Watalii Laki moja wanaofika Visiwani Zanzibar kila mwaka. Karakana ya TEMESA Vingunguti Dar es Salaam imeendelea kudhihirisha umuhimu wa Watanzania kufanya utalii wa ndani kwakua utamaduni huo una manufaa makubwa kwa Taifa ikiwemo kukuza pato la Taifa kupitia tozo mbalimbali zinazotozwa ndani ya Hifadhi hizo lakini pia inawaongezea ufahamu watumishi kuhusu vivutio mbalimbali vya Kiutalii ambavyo vipo ndani ya nchi yao.