TEMESA YASHUSHA NEEMA KWA WAKAZI WA KILWA KISIWANI NA LINDI KITUNDA

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imeshusha neema kwa wakazi wa Kilwa Kisiwani na Lindi Kitunda baada ya leo kuwapelekea Boti mpya kwa ajili ya kubeba abiria na kubeba wagonjwa (Ambulance Boat). Boti hizo mbili, MV. LINDI itakayotoa huduma ya kubeba abiria kati ya Lindi na Kitunda na MV. LUKILA itakayokuwa ikitoa huduma ya kubeba wagonjwa katika eneo la Kilwa Kisiwani, zote zimejengwa na kampuni za kizalendo kutoka Tanzania za Songoro Marine Transport Boatyard ya jijini Mwanza iliyojenga boti ya kubeba wagonjwa (Ambulance Fibre Boat) na kampuni ya Sam & Anzai Boat Builders Co. Ltd ya Dar Es Salaam iliyojenga boti ya abiria (Passenger Fibre Glass Boat) zimekabidhiwa rasmi leo katika hafla fupi iliyofanyika katika eneo la feri Mkoani Lindi mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Zainab Telack.