KATIBU MKUU WA WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI ZANZIBAR ASISITIZA TAASISI ZA SERIKALI KUWEKEZA KATIKA MIFUMO YA KISASA YA KIDIJITALI
Posted On: September 21, 2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Ali Bakar, amezitaka taasisi za Serikali kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya kidijitali katika kutekeleza majukumu ili kurahisisha utendaji wa kazi, Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo leo tarehe 21 Septemba, 2026 wakati alipotembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani, yanayofanyika katika Viwanja vya Kijiji cha Ishirini na Moja, Mkoani Tanga.
Akiwa bandani hapo, Mhandisi Bakar ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia yana nafasi muhimu katika kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi na kuboresha huduma kwa wananchi. Aidha, Mhandisi Ali amewataka wataalamu kutoka Karakana Kuu ya Matengenezo ya Magari ya Serikali ya Zanzibar kutembelea TEMESA kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu teknolojia za kisasa za matengenezo ya magari pamoja na matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Matengenezo ya Magari (MUM).
“Niwatake wataalamu wetu wa karakana kuu ya Matengenezo ya magari Zanzibar kutembelea banda la TEMESA ili kujifunza, kufanya mashirikiano ya kiutendaji na kubadilishana uzoefu katika matumizi ya kidigitali,” amesema Mhandisi Bakar.
Aidha, akiwa katika banda la TEMESA Mhandisi Bakar ameweza kujionea shughuli, huduma na teknolojia mbalimbali zinazotumika na Wakala katika utekelezaji wa majukumu yake, hususani katika eneo la matengenezo na usimamizi wa magari pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani (World Maritime Day 2026) yanafanyika mkoani Tanga kuanzia Septemba 21 hadi 24, 2026 na yanaongozwa na kaulimbiu ““Kutoka sera hadi utekelezaji: kuimarisha ubora katika sekta ya Usafirishaji Majini” inayosisitiza utekelezaji wa sera, sheria, mikakati na miongozo katika kuimarisha usalama wa usafiri majini, ustawi wa mabaharia na maendeleo ya sekta ya bahari.