UKARABATI KIVUKO MV. KILAMBO WAKAMILIKA; CHASUBIRI KIBALI KUTOKA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA ILI KUTOA HUDUMA
Posted On: September 19, 2026
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Mhandisi Lukombe King’ombe, tarehe 17 Septemba 2026 ametembelea na kukagua maendeleo ya kivuko cha MV. KILAMBO kilichokuwa kinatoa huduma kati ya eneo la Kilambo Mtwara, Tanzania na Namoto nchini Msumbiji).
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mhandisi King’ombe amesema kivuko MV. KILAMBO kilisimama kutoa huduma kwa muda kutokana na sababu za kiusalama, hasa upande wa Msumbiji hali iliyoilazimu Serikali kukisimamisha mpaka pale hali ya usalama itakaporejea na kwa sasa usalama umerejea na hivyo Serikali imeona ni wakati sahihi wa kurejesha huduma hiyo kwa kuwa wakazi wa maeneo hayo ya mpakani wanahitaji huduma hiyo ya kivuko.
“Tumefanya ukaguzi wa rampu pamoja na kivuko chetu cha Kilambo ambacho kilikuwa imesimama kutoa huduma kutokana na sababu za kiusalama upande wa Msumbiji. tayari tumekifanyia marekebisho kwa kurudia rangi kwasbabu kilikuwa kimesimama kwa muda mrefu bila kufanya kazi, tumekisafirisha kutoka Mtwara mjini kwenda mpaka Kilambo kinapotakiwa kutoa huduma na kipo tayari kwenye gati lake, kwa sasa tunasubiri taratibu za mwisho za ukaguzi wa kiusalama upande wa Msumbiji pamoja na miundombinu yake ili kianze kutoa huduma mara moja tutakapopata kibali kutoka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mtwara,” amesema Mhandisi King’ombe.
Mhandisi King’ombe ameongeza kuwa sasa kivuko kimekamilika na kiko tayari kufanya kazi na mabaharia wote wako katika eneo la kivuko wakisubiri kibali kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ya kivuko.
Aidha, Mhandisi King’ombe ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania wanasubiri pia utaratibu wa kibali cha usalama kutoka kwa mamlaka husika upande wa Serikali ya Msumbiji ambao wamekutana tayari kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa miundombinu ya mji na bandari yake upande wa Namoto Msumbiji na mara watakapokamilisha kivuko hicho kitarejea kutoa huduma.
“Tunasubiri pia kibali cha usalama kutoka upande wa wenzetu wa mamlaka za Serikali ya Msumbiji ili kivuko kianze kutoa huduma kati ya Kilambo na Namoto, upande wa Msumbiji bado wanaendelea na kazi ya kurekebisha miundombinu, pindi tu miundombinu itakapokamilika, kivuko kitaanza kutoa huduma kwa sababu sasa kipo tayari,” amefafanua Mhandisi King’ombe.
Kivuko cha MV.KILAMBO ni muhimu kwa biashara na usafiri wa abiria kati ya Tanzania na Msumbiji kupitia mpaka wa Kilambo–Namoto. Kivuko MV. KILAMBO kinao uwezo wa kubeba tani 50, abiria 100 na magari madogo 6.