TEMESA YAKABIDHIWA TUZO YA HESHIMA KUFUATIA UDHAMINI WA KONGAMANO LA MADEREVA
Posted On: September 19, 2026
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umekabidhiwa Tuzo ya Heshima kwa kutambua mchango wake katika kufanikisha Kongamano la Tano la Madereva wa Serikali Tanzania lililofikia tamati Septemba 18, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Tuzo hiyo iliyotilewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Mhe. Badria Atai Masoud, na kupokelewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Bi. Saphinaeli Mapesa, imeonesha ishara ya kutambua mchango, ushirikiano na udhamini wa TEMESA katika kongamano hilo lililowakutanisha madereva wa Serikali na wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala yanayohusu taaluma ya udereva, usalama barabarani, matumizi sahihi ya magari ya Serikali pamoja na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa magari.
Ushiriki wa TEMESA katika kongamano hilo unaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya TEMESA na wadau mbalimbali, sambamba na kutoa fursa ya kuendelea kutangaza na kuelimisha Umma kuhusu huduma za kiufundi na kihandisi zinazotolewa na TEMESA.