WADAU TEMESA MBEYA WANOLEWA MAFUNZO YA MFUMO WA MUM

News Image

Posted On: May 31, 2025

Wadau wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Mbeya wamepatiwa mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM), kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya matumizi sahihi ya mfumo huo pamoja na kukusanya maoni kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma zake nchini.

Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 22 Mei 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Tughimbe Hotel mkoani humo, yakiendeshwa na Mhandisi Pongeza Semakuwa, Meneja wa Kikosi cha Umeme TEMESA na Mratibu wa Mfumo huo kwa ngazi ya kitaifa ambapo Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wamiliki wa gereji teule pamoja na watumishi kutoka taasisi mbalimbali za serikali zinazopokea huduma kutoka TEMESA.

Akieleza umuhimu wa mfumo huo, Mhandisi Pongeza amesema mfumo wa MUM umeundwa na Serikali ili kupunguza muda, kuwezesha bei za huduma kufanana katika ofisi zote za TEMESA nchini na kuweka uwazi baina ya TEMESA na taasisi inazozihudumia hivyo mfumo huo ni muhumi kwa pande zote mbili kwani utarahisisha uwazi na kutunza kumbukumbu ukilinganisha kipindi cha awali.

“Mfumo wa MUM umeundwa ili kuongeza uwazi, kupunguza muda wa utekelezaji wa kazi na kuhakikisha bei ya huduma inafanana nchi nzima. Ni chombo muhimu kwa uwajibikaji wa pande zote mbili." Amesema Mhandisi.

Aidha Mhandisi Pongeza amewasihi wadau wa TEMESA kuunga mkono juhudi za mabadiliko yanayoendelea ili kuchochea ufanisi na uwazi katika huduma zake.

Fundi Makangavuke kutoka TEMESA Mbeya, Bw. Olesi Nakapete, amesema mfumo wa MUM utawarahisishia kukusanya mapato yao kwa wakati bila kusumbuana na wateja wao ukilinganisha na awali pia amewasihi mafundi wenzake kufanyakazi kwa kujiamini.

"Kupitia MUM, tutaweza kufuatilia mapato yetu kwa ufanisi zaidi na kuwahudumia wateja kwa wakati bila usumbufu. Mafundi tunapaswa kutumia mfumo huu kwa kujiamini."

Bi. Suma Mwambela kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) amesema Kupitia MUM, wanaweza kuona hatua kwa hatua kila kazi inavyoendelea hadi kukamilika ambapo hatua hii imewapa urahisi mkubwa kazini.

“Kupitia MUM, tunaweza kuona kila hatua ya kazi kwa uwazi hadi inakamilika. Hii inatusaidia kupanga bajeti na muda vizuri."

Naye Dr. Alex kasimba kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama amesema wamekua wakiomba huduma kwenye mfumo kwa zaidi ya miezi miwili hadi sasa na wamekuwa wakipatiwa huduma nzuri kwa wakati stahiki.

“Mfumo huu umeleta mageuzi makubwa. Hii ni hatua ya kisasa inayowiana na dira ya serikali ya kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma ni matumaini yetu mfumo huu utaturahisishia zaidi muda wa utendaji kazi."Amesisitiza Dr. Kasimba.