TEMESA YAWAJENGEA MAMENEJA UWEZO WA MUM
Posted On: September 19, 2026
Mameneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kutoka mikoa mbalimbali nchini wamejengewa uwezo kuhusu matumizi sahihi na yenye ufanisi ya Mfumo wa Usimamizi wa kazi za Matengenezo (MUM), unaolenga kuboresha usimamizi wa kazi za matengenezo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Mafunzo hayo yamefanyika Septemba 17, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za TEMESA Makao Makuu, Tambukareli jijini Dodoma, yakiongozwa na Mhandisi Pongeza Semakuwa. Mafunzo hayo yamejikita katika kuwawezesha mameneja kuelewa na kutumia ipasavyo mfumo huo katika kusimamia shughuli za matengenezo, kufuatilia utekelezaji wa kazi na kuhakikisha taarifa muhimu za kiutendaji zinaingizwa na kutumika kwa usahihi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhandisi Semakuwa amesisitiza umuhimu wa mameneja kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya MUM, kwa kuwa mfumo huo ni nyenzo muhimu katika kuimarisha uwazi, ufuatiliaji na ufanisi wa kazi za matengenezo ndani ya TEMESA. Ameeleza kuwa matumizi sahihi ya mfumo huo yatauwezesha Wakala kuwa na taarifa sahihi na kwa wakati, hivyo kusaidia katika kufanya maamuzi na kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi.