TEMESA YATOA MAFUNZO KWA WAKUU WA KARAKANA KUIMARISHA UBORA NA UFANISI WA HUDUMA

News Image

Posted On: October 30, 2026


Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umeendesha mafunzo kwa wakuu wa karakana kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha ujuzi, kuongeza tija na kuboresha ubora na ufanisi wa huduma za matengenezo ya magari.

Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 27 Oktoba, 2026 katika Karakana ya TEMESA Mkoa wa Dodoma na kufunguliwa na Mhandisi Billy Munishi, Meneja wa Karakana Mkoa wa Dodoma, ambaye amesisitiza umuhimu wa kusimamia shughuli za karakana kwa ufanisi ili kuongeza tija na kuhakikisha wateja wanapata huduma bora.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhandisi Munishi amesema ni muhimu kuhakikisha kila kazi ya matengenezo inafanyika kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa, magari yanakamilishiwa matengenezo kwa wakati na wateja wanapata huduma zinazokidhi mahitaji yao.

“Ni muhimu kuhakikisha kila kazi inafanyika kwa ubora unaotakiwa, magari yanatengenezwa kwa wakati na wateja wanapata huduma bora zinazokidhi mahitaji yao,” amesema Mhandisi Munishi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutumia vipuri vyenye ubora unaotakiwa na kuzingatia uadilifu katika kushughulika na wazabuni, akieleza kuwa ubora wa vipuri una mchango mkubwa katika uimara wa matengenezo, usalama wa magari na kupunguza gharama zinazoweza kusababishwa na hitilafu zinazojirudia.

Vilevile, amewahimiza washiriki kuimarisha matumizi ya ujuzi na uwezo wa ndani wa karakana katika kutatua changamoto za kiufundi, kwa kuhakikisha hitilafu za magari zinatambuliwa na kutatuliwa kikamilifu tangu mara ya kwanza ili kupunguza muda wa magari kukaa karakana na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Baada ya mafunzo ya darasani, washiriki walifanya ziara ya mafunzo kwa vitendo katika vitengo mbalimbali vya Karakana ya TEMESA Dodoma. Katika ziara hiyo, walijifunza hatua mbalimbali za utoaji huduma, zikiwemo upokeaji wa magari, ukaguzi, utambuzi wa hitilafu, uandaaji wa makadirio ya gharama na utekelezaji wa matengenezo kwa kutumia mitambo na vifaa vilivyopo.

Mafunzo hayo ya siku moja yalijumuisha masuala ya usalama kazini, matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga na tathmini ya ziara ya mafunzo kwa vitendo, kwa lengo la kuhakikisha washiriki wanaimarisha uelewa na uwezo wao katika kusimamia shughuli za karakana kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.