PROFESA SHEMDOE AFUNGUA MAONESHO YA MWANAKATAVI, TEMESA YASHIRIKI
Posted On: October 30, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amefungua Maadhimisho ya Tano ya Wiki ya Mwanakatavi 2026, yanayofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mizengo Pinda, Kata ya Kabungu, Wilaya ya Tanganyika, Mkoani Katavi. Maadhimisho hayo yanalenga kutoa fursa kwa wananchi, wakulima, wafugaji, wavuvi, wajasiriamali na wawekezaji kufahamu shughuli na huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali, kutangaza bidhaa zao, kujifunza teknolojia mpya, kutafuta masoko na kubaini fursa za uwekezaji kwa ajili ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Katavi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Prof. Shemdoe amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kujifunza mbinu na teknolojia mpya zitakazowasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo, ufugaji na biashara, kuongeza tija na kipato, na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
“Tumieni jukwaa hili kujifunza teknolojia mpya zilizopo hapa ili wazalishaji wapate mbinu mbalimbali zitakazoongeza tija katika kazi zao na kuwawezesha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,” amesema Prof. Shemdoe.
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazoshiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake za kiufundi, kuimarisha uelewa wa umma na kuhamasisha matumizi ya huduma zinazotolewa. Maadhimisho hayo ya Tano ya Wiki ya Mwanakatavi 2026 yalianza tarehe 25 na yataendelea hadi tarehe 31 Oktoba 2026, yakibeba kaulimbiu isemayo: “Katavi Yetu, Talii, Wekeza, Imarisha Uchumi Kutekeleza Dira ya Taifa 2050.”